Ruth Machocho, mwenye umri wa miaka 32, ni mmoja wa waathirika wa ajali za barabarni nchini Kenya. Picha/TRT Afrika. 

Fathiya Bayusuf

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Huku dunia ikianza mwaka mpya wa 2024, sherehe za kufunga mwaka mara nyingi zimekuwa zikiambatana na taarifa mbaya za ongezeko la ajali za barabarani.

Moja kati ya simulizi za kusikitisha ni ile ya Ruth Machocho, mwenye umri wa miaka 32, kutoka eneo la Kiembeni, nje kidogo na mji wa Mombasa nchini Kenya. Kumbukumbu ya tarehe 30 mwezi Aprili 2023, inachimbika akilini mwake kama alama ya siku ambayo maisha yake yalibadilika milele. Ruth alikuwa anarudi nyumbani baada ya kuhudhuria tamasha la rafiki yake, majira ya asubuhi, lakini kile ambacho hakuwahi kukitarajia kilitokea.

Idadi kubwa ya vifo katika nchi za Afrika inasababishwa na ajali za barabarani. Picha/TRT Afrika.

"Nikiwa eneo la Nyali, kando ya barabara kuu ya Mombasa - Malindi, ghafla gari la mizigo lililokuwa linakuja kwa kasi lilinigonga pamoja na dereva wangu wa pikipiki, na kusababisha ajali mbaya. Kwa bahati mbaya, dereva wa pikipiki alipoteza maisha yake, huku mimi nikipitia upasuaji na hatimaye kukatwa mguu wa kushoto. Hii ilikuwa ni ajali isiyotarajiwa," anasimulia Ruth, akiwa shuhuda na muathirika wa ajali.

Safari ya Ruth iligeuka kuwa changamoto kubwa, ikimuathiri sana kimwili na kiakili. Gharama kubwa ya matibabu ilijitokeza kama kizingiti kikubwa, kikifanya upatikanaji wa huduma bora ya afya kuwa jambo lenye changamoto. Anaeleza jinsi hali hiyo ilivyomfanya apambane na ukweli wa kuwa mlemavu, na jinsi matumizi ya mguu bandia yalivyoleta mabadiliko makubwa katika maisha yake.

"Lazima ukubali matokeo, ijapokuwa si rahisi, hasa unapogeuzwa kuwa mlemavu ghafla. Matumizi ya mguu bandia yanakuja na changamoto zake, kuanzia kujifunza jinsi ya kutembea tena hadi kushughulika na vikwazo vya kila siku. Hata kuoga kunakuwa safari ndefu, na mara nyingine unajikuta unavaa viatu popote ulipo, hata nyumbani," anaelezea Ruth, akiongeza muktadha wa maisha yake ya sasa.

Ajali za barabarani mara nyingi zinachangiwa na ukiukaji wa sheria na kanuni za barabarani. Picha/TRT Afrika. 

Ajali iliyokuwa inaogofya ilimlazimu kutumia fimbo ya kutembea, ikipunguza uwezo wake wa kufanya kazi na kusimamia mahitaji ya familia yake. Ruth alijikuta akihitaji msaada wa ndugu, jamaa, na marafiki, waliomsaidia si tu kifedha bali pia kiroho na kisaikolojia.

Ajali za barabarani nchini Kenya na maeneo mengine ya bara zimegeuka kuwa janga la kibinadamu, zikisababisha machungu na majonzi kwa familia nyingi. Athari zake hazitambui mipaka, zikiongeza idadi ya watoto yatima, kuwaacha baadhi wakiwa wajane, na wengine wakipoteza wategemezi wa familia zao. Hii ni pamoja na maelfu ya waathirika wanaoendelea kupambana na majeraha, kama ilivyo kwa Ruth, ambaye anakabiliana na kumbukumbu zenye uzito kutokana na ajali iliyokaribia kumgharimu maisha.

Vipul Patel, mtaalamu wa masuala ya usalama barabarani, anasisitiza kuwa tatizo la ajali za barabarani ni la kiwango kikubwa barani Afrika. Gharama zinazohusiana na ajali, kama matibabu, bima, masuala ya polisi, na mahakamani, zinaleta mzigo mkubwa kwa serikali na jamii kwa ujumla. Analinganisha tatizo hili na magonjwa mengine kama malaria na COVID-19, akisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu ya kudumu.

George Kashmiri, Mkuu wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani- Trafiki, Pwani ya Kenya. Picha/TRT Afrika.  

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira UNEP, Barani Afrika, takriban asilimia 20 ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani duniani vinatokea, huku idadi ya magari ikiwa chini ya asilimia 3 ya jumla ya magari duniani. Hii inaonyesha wazi kuwa changamoto zinazokabili usalama barabarani zinahitaji kushughulikiwa kwa ufanisi. Miundombinu duni, mipango mibovu ya mijini, na uendeshaji mbaya wa magari ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia hali hii.

Huko Kenya, takwimu kutoka Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani zinaonyesha kuwa idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani imepungua kidogo mwaka wa 2023, lakini bado ni ya kutia wasiwasi. Watembeaji kwa miguu bado wanaendelea kuwa wahanga wakubwa. Ajali nyingi hutokea wakati wa mwishoni mwa juma na kipindi cha usiku, huku madereva walevi na uendeshaji hatarishi ikiwa ni sababu kubwa.

George Kashmiri, Mkuu wa Trafiki wa Pwani ya Kenya, anaeleza changamoto zinazochangia ajali hizi, huku akibainisha kuwa watu wengine hawana uzoefu wa kuendesha gari kwa muda mrefu, na wengine wanachoka, jambo linaloweza kusababisha uendeshaji mbaya.

Anasema, "Pia, matumizi ya magari ya kukodisha bila uzoefu na magari mabovu ni mambo mengine yanayochangia ajali. Ulevi wakati wa sherehe pia ni mojawapo ya sababu kuu za ajali.”

Vipul Patel, mtaalamu wa masuala ya usalama barabarani nchini Kenya. Picha/TRT Afrika. 

Vipul Patel, anapendekeza kuboresha miundombinu ya barabara, kutoa elimu ya usalama wa barabarani, na kuimarisha huduma za afya ili kupunguza mzigo unaotokana na ajali. Pia, anahimiza uwekezaji katika sera za bima na mikakati ya kijamii kusaidia waathirika na familia zao kukabiliana na changamoto za kiuchumi.

Mtaalamu huyu anasisitiza pia jukumu la vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu usalama barabarani, na anatoa wito kwa serikali kuongeza fedha kwenye masuala ya usalama barabarani.

Anasema, "Inaweza kuwa taa za barabarani hazifanyi kazi, labda barabara hazipakwi rangi, na hata hata alama za wapita kwa miguu pundamilia haijawekwa kila mahali, pamoja na ukosefu wa ishara za barabarani. Tunatambua kuwa yapo mapungufu hayo, lakini jukumu ni la raia kuhakikisha wanatii sheria za barabarani, kwa sababu wanapozingatia, wanachangia kuokoa maisha. Tunataka serikali iongeze fedha kwenye masuala ya usalama barabarani ili vitengo husika viweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,"

George Kashmiri, Mkuu wa Trafiki wa Pwani ya Kenya, anatoa maoni yake juu ya umuhimu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva, na kuweka vifaa vya kupimia ulevi kwenye barabara kuu.

Wito unaendelea kutolewa kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za barabarani. TRT Afrika. 

Hata hivyo, licha ya juhudi za kuboresha usalama barabarani, waathirika kama Ruth bado wanapambana miezi baada ya ajali, na wito unaendelea kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za trafiki. Wananchi wanasisitiza pia juu ya umuhimu wa serikali kuchukua hatua kali dhidi ya madereva walevi, magari mabovu, na kuhakikisha kuwa taa na ishara zote za trafiki zinatekelezwa barabarani. Maoni kutoka kwa Benjamin Mwajambo na Shaaban Rama yanatoa mwanga wa jinsi jamii inavyoweza kuchangia usalama barabarani.

TRT Afrika