Simanzi yatawala katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mjini Arusha Tanzania wakati wa shughuli baadhi ya kuaga miili ya waathirika wa ajali iliyohusisha gari la mizigo, na magari madogo 3. Ajali hiyo iliyotokea Februari 24, 2024 iliua jumla ya watu 25.
Kati ya hao, walioagwa hii leo ni 11. Wakati huo huo, pia kuna raia 10 wa kigeni ambao walipoteza maisha yao. Taarifa zinasema, raia hao wa kigeni walikuwa kwenye ziara ya mafunzo iliyoisha Februari 23, na walikuwa wanajiandaa kurudi katika nchi zao kabla ya kukutwa na ajali hiyo.
Mbali na viongozi wengine wa mkoa, shughuli hiyo pia imehudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania, Pindi Chana akiongoza mamia ya waombolezaji.
Ajali hiyo ilihusisha magari manne, baada ya lori lililopata hitilafu kwenye mfumo wake wa breki na kuparamia magari mengine madogo matatu.
"Tutaendelea kuwa karibu na familia hizi hadi pale tutakapokamilisha taratibu za mazishi haya,poleni sàna familia," alisema John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Mara ya mwisho simanzi kugubika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilikuwa ni mwaka 2017, wakati wa kuwaaga wanafunzi 33 kutoka shule ya Lucky Vincent waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Karatu, mkoani Arusha.