Rais wa Kenya, William Ruto amempandisha cheo na kisha kumteua Charles Kahariri kuwa mkuu mpya wa majeshi wa nchi hiyo.
Jenerali Kahariri, ambaye anachukua nafasi ya Francis Ogolla aliyefariki dunia Aprili 18 katika ajali ya Helikopta, alikuwa na cheo cha Luteni Jenerali na makamu Mkuu wa Majeshi wa Kenya, kabla ya uteuzi huo.
Kwa sasa, Kahariri ndio afisa jeshi pekee mwenye cheo cha nyota nne, kulingana na madaraka ndani ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).
Mzunguko wa Madaraka
Nafasi ya Ukuu wa Majeshi nchini Kenya ni ya mzunguko, kulingana na utaratibu wa nchi hiyo.
Jenerali Kahariri anatokea Jeshi la Majini, huku mtangulizi wake Ogolla, akiwa mwana anga.
Tazama Zaidi ili kufahamu nafasi za kijeshi Afrika Mashariki.
Safari ya Kahariri Jeshini
Kabla ya uteuzi wake, Jenerali Kahariri alikuwa naibu kamanda wa Chuo cha Taifa cha Kijeshi cha nchi hiyo.
Pia aliwahi kuwa naibu kamanda wa Jeshi la Maji nchini Kenya.
Kulingana na sheria ya KDF, Mkuu wa Majeshi wa Kenya anahudumu kwa kipindi cha miaka minne na kustaafu pindi afikishapo miaka 62.
Hata hivyo, sheria hiyo inampa mamlaka Rais, kwa mapendekezo ya Baraza la Taifa la Ulinzi, kumuongezea muda Mkuu wa Majeshi kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja.
Mbali na umri, uteuzi wa Mkuu wa Majeshi nchini Kenya huzingatia nafasi alizohudumu afisa huyo kabla ya kuvaa nyota nne mabegani mwake..