Jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakipigana vita tangu katikati ya Aprili 2023 ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya watu 20,000. / Picha: Reuters

Jeshi la Sudan liliuteka mji wa Soba, mashariki mwa mji mkuu Khartoum, siku ya Jumatatu katika harakati za hivi karibuni za kijeshi dhidi ya vikosi vya RSF.

Kundi la Sudan Shield Forces linaloshirikiana na jeshi limesema kuwa vikosi vyake vimechukua udhibiti wa eneo hilo.

Kundi hilo liliweka video ikimuonesha kamanda wake Abu Agla Keikel ndani ya kituo cha polisi mjini humo.

Keikel alijiondoa kutoka kwa RSF mnamo Oktoba 2024.

Harakati za RSF kupigwa kikomo

Jeshi pia lilithibitisha katika taarifa yake kwamba vikosi vyake vimekamata daraja la kimkakati la Soba kwenye Blue Nile na mji wa Soba baada ya mapigano na wapiganaji wa RSF.

Wanaharakati wa mitandao ya kijamii waliweka video kadhaa za vikosi vya jeshi kwenye daraja kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mapigano Aprili 2023.

Kutekwa kwa eneo la daraja kungezuia harakati za vikosi vya RSF katika maeneo ya Mashariki ya Nile, ambapo Daraja la al-Manshiya juu ya Blue Nile limebaki tu kwa vikundi vya waasi RSF. Daraja hili linaunganisha eneo la Nile Mashariki na vitongoji vya mashariki vya Khartoum.

Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan pia vilisonga mbele magharibi mwa Mto Blue Nile kuelekea eneo la Al-Baqir, ambalo ni lango la kuingilia Khartoum kutoka Jimbo la Al-Jazirah.

Maendeleo zaidi

Hatua hizi mpya zimekuja wakati jeshi likiendelea kuunganisha mafanikio yake ya kijeshi katika nyanja nyingi huko Khartoum na eneo la Nile Mashariki katika Jiji la Bahri, ngome kuu ya RSF.

Siku ya Jumapili, jeshi la Sudan liliuteka mji wa Alkotainh katika Jimbo la White Nile kusini mwa Sudan.

Alkotainh, kilomita 100 kusini mwa Khartoum, ulikuwa mji pekee unaodhibitiwa na RSF kusini mwa Sudan.

Kundi la wanamgambo bado linadhibiti majimbo manne kati ya matano ya Darfur, wakati kaskazini na mashariki mwa Sudan bado haijaathiriwa na mapigano.

Maeneo ya kimkakati

Katika Jimbo la Khartoum, ambalo lina miji mitatu, jeshi sasa linadhibiti 90% ya Bahri kaskazini, sehemu kubwa ya Omdurman upande wa magharibi, na 60% ya Khartoum ya kati, ambapo ikulu ya rais na uwanja wa ndege wa kimataifa unapatikana. Vikosi vya jeshi vimekaribia kuzunguka maeneo haya ya kimkakati, wakati wapiganaji wa RSF wakiwa bado wamejikita katika vitongoji vya mashariki na kusini.

Jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakipigana vita tangu katikati ya Aprili 2023 ambavyo vimesababisha vifo vya watu 20,000 na wengine milioni 14 kuyahama makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa na mamlaka za kikanda.

Utafiti kutoka vyuo vikuu vya Marekani, hata hivyo, unakadiria idadi ya vifo kuwa karibu 130,000.

Wito wa kimataifa na Umoja wa Mataifa wa kusitisha vita unazidi kuongezeka, huku kukiwa na onyo la matatizo makubwa kwa raia wakati mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula. Mzozo huo umeenea hadi katika majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan.

TRT Afrika