Jeshi la Sudan limesema linaratibu juhudi za kuwaondoa wanadiplomasia kutoka Marekani, Uingereza, China na Ufaransa nje ya nchi kwa ndege za kijeshi, huku mapigano yakiendelea katika mji mkuu, ukiwemo uwanja wake mkuu wa ndege.
Nchi imekumbwa na mapigano ya umwagaji damu tangu wiki iliyopita ambayo yameua zaidi ya watu 400 hadi sasa, kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO.
Nchi za kigeni zimejaribu bila mafanikio kuwarejesha makwao raia wao, kazi inayoonekana kuwa hatari sana kwani mapigano kati ya jeshi la Sudan na kundi pinzani la wanamgambo wenye nguvu yamepamba moto ndani na karibu na Khartoum, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya makazi.
Uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa karibu na katikati mwa mji mkuu umekuwa ukilengwa kwa makombora makubwa huku kundi la wanamgambo Rapid Support Forces, RSF, likijaribu kuchukua eneo hilo, na hivyo kutatiza mipango ya uhamishaji.
Huku anga ya Sudan imefungwa, mataifa ya kigeni yamewaamuru raia wao kujihifadhi hadi watakapoweza kujua mipango ya kuwahamisha.