Rais wa Uganda Yoweri Museveni, siku ya Alhamisi amezindua ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR), mradi unaotekelezwa na kampuni ya Uturuki ya Yapi Merkezi.
Pindi utakapokamilika, reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani 1,000 za mzigo kwa wakati mmoja.
Kulingana na Rais Museveni, mradi huo utachochea biashara kati ya Uganda na nchi nyingine za jirani pamoja na sekta zingine za kiuchumi.
"Kiwango cha biashara barani Afrika kinashuka kwa asilimia 40 kutokana na ubovu wa miundombinu, huku gawio lake likiwa chini ya asilimia 15 wakati kwa mabara mengine inafikia asilimia 40 hadi 60," alisema Rais Museveni.
Kuchochea biashara ya kanda
Museveni amesema kuwa kutokuunganika vizuri kwa miondombinu barani Afrika, kunatatiza biashara, na hivyo kulifanya bara hilo kuendelea kutegemea masoko ya nje.
"Kwa kuunganisha Uganda na ukanda wote, tunaazimia kuchochea biashara ya kikanda, huku tukifanya biashara ndani ya Afrika," aliongeza.
Kwa mujibu wa Rais Museveni, usafiri kati ya Mombasa na Kampala utatumia saa 10, tofauti na saa 14, pindi mradi huo utakapokamilika.
Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Uganda, Fatih Ak, alisema kuwa Ankara itaendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Uganda.