Wizara ya Mambo ya Nje ya Haiti imemuita balozi wa Ufaransa Antoine Michon siku ya Alhamisi kumlalamikia kuhusu "matamshi yasiyokubalika" ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika mkutano wa G20.
Macron, alipokuwa akizungumza katika hafla hiyo wiki hii nchini Brazil, alilishutumu Baraza la mpito la nchi hiyo ya Caribbean kwa kile alichokiita "wajinga kabisa" kwa kumfukuza kazi Waziri Mkuu wake.
"Ni wajinga kabisa. Hawakupaswa kamwe kumfukuza kazi," aliongeza, akimaanisha kutimuliwa kwa Waziri Mkuu wa zamani Garry Conille na Baraza la Mpito la Haiti siku chache zilizopita.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Haiti ilisema kuwa Balozi wa Ufaransa Antoine Michon ameitwa kufuatia matamshi hayo, ambayo Wizara hiyo iliyataja kuwa "sio kirafiki na yasiyofaa."
Matamshi hayo yenye utata yalizua malalamiko kutoka kwa mamlaka ya Haiti siku ya Alhamisi.
Conille, ambaye aliteuliwa na Baraza hilo kushika wadhifa huo mwezi Mei, alifanya kazi kwa miaka kadhaa katika Umoja wa Mataifa kabla ya kurejea nchini kuandaa njia ya uchaguzi wa urais mwaka ujao na kurejesha utulivu.
Baada ya taarifa ya kufutwa kwake kufuatia mzozo wa madaraka na baraza la madiwani kuhusu udhibiti wa serikali, alisema hatua ya kumuondoa ni kinyume cha katiba. Conille alibadilishwa Novemba 11 na aliyechukua nafasi yake hivi sas ni mfanyabiashara Alix Didier Fils Aime.
Matamshi hayo yenye utata yalizua maandamano kutoka kwa mamlaka ya Haiti siku ya Alhamisi.
Macron aliahidi Alhamisi kwamba "Ufaransa haitatazama kwa kando wakati wa mzozo," na kuongeza "kutakuwa na msimamo mmoja wakati wa janga, iwe ni Haiti, Venezuela au popote Uropa."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Haiti ilisema katika mkutano huo, balozi wa Ufarasa, Michon aliahidi kuwa Ufaransa itasimama upande wa Haiti kusaidia kurejesha usalama na kufanya uchaguzi.
Ufaransa imeahidi kuchangia Euro milioni 4 (dola milioni 4.18) kwa hazina ya Umoja wa Mataifa ambayo inafadhili ujumbe wa usalama unaonuiwa kurejesha usalama nchini Haiti.