Wapiga kura nchini humo wataelekea kwenye uchaguzi Julai 15 / Picha kutoka RPF 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Rwanda imetoa orodha ya mwisho ya wapiga kura, ikionyesha kwamba watu milioni 9.7 wanastahili kupiga kura mwezi Julai.

Raia wa Rwanda walio nje ya nchi watapiga kura zao kwa rais na wabunge 53 mnamo Julai 14 katika balozi za nchi hiyo huku wapiga kura nchini humo wakielekea kwenye uchaguzi Julai 15.

Ikiwa na zaidi ya watu milioni 13, orodha ya mwisho iliyotolewa kabla ya daftari la wapiga kura kufungwa Jumamosi, ilionyesha vijana milioni 3.7 wanastahili kupiga kura.

"Wanyarwanda wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wakiwa na vitambulisho vya taifa wanaonekana kwenye orodha. Wapiga kura watatakiwa kuwasilisha vitambulisho vyao vya kitaifa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili waruhusiwe kupiga kura tofauti na hapo awali wakati kadi ya mpiga kura ilipotumika," mwenyekiti wa tume hiyo Oda Gasinzigwa. aliambia televisheni ya taifa siku ya Jumapili.

President Paul Kagame campaigns for July 15 Presidential elections 2024 photo by RPF

Tume hiyo pia imesema vituo 2,591 vya kupigia kura vimetengwa ili kuwezesha uchaguzi huru wa haki.

Kampeni zimepamba moto nchini Rwanda.

Wagombea wa kiti cha urais wameanza kampeni katika sehemu tofauti za nchi kwa lengo la kuuza sera ili kuwashawishi wananchi kuwapigia kura katika uchaguzi mkuu wa 15 Julai 2024.

Rais Paul Kagame wa Rwanda anatetea nafasi yake katika uchaguzi huu baada ya kuteuliwa na chama chake kusimama katika kinyanganyiro hicho. Paul Kagame aliyezaliwa 1957 ni kiongozi wa zamani wa jeshi la Rwanda ambaye sasa ni mwanasiasa.

Aliongoza vikosi vya Rwandan Patriot Front (RPF) na kushinda vikosi vya Wahutu waliokuwa na msimamo potovu na hapo kumaliza mauaji ya kimbari ya 1994. Mwaka 2000 akawa rais wa Rwanda.

Mgombea mwengine ni Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda/ picha Frank Habineza

Kagame aliwahi kuwa waziri wa ulinzi na makamu wa rais, na kisha kushika wadhifa wa urais mwaka 2003, akishinda kwa asilimia 95 ya kura.

Katika kura ya maoni ya mwaka 2015, Wananchi wa Rwanda walipiga kura kuondoa ukomo wa mihula miwili. Kagame anaweza kusalia madarakani hadi 2034 ikiwa atashinda kwa muhula wa miaka mitano mwaka ujao na kisha mwingine.

Mgombea mwengine ni Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda, aliyezaliwa 1977.

Habineza amewahi kuwa msaidizi maalumu wa waziri chini ya Rais Kagame na amefanya kazi katika mashirika mawili ya habari. Mnamo 2010, Habineza alilazimika kukimbia Rwanda na kutafuta hifadhi nchini Sweden, ambako aliishi hadi 2012.

Baada ya kurejea nyumbani hatimaye alifanikiwa kusajili rasmi chama cha Democratic Green Party of Rwanda mnamo Agosti 2013. Aligombea katika uchaguzi wa urais wa 2017, na kupata chini ya asilimia moja ya kura huku Kagame akipata ushindi wa 99%.

Habineza pia aligombea katika uchaguzi wa wabunge wa 2018, chama chake kikapata nafasi mbili bungeni.

Philippe Mpayimana ni mgombea binafsi / Picha:  Philippe Mpayimana

Mgombea wa tatu ni Philippe Mpayimana wenye miaka 54, ambaye ni mgombea binafsi na mwanahabari kitaaluma, ambaye aliishi Ulaya kabla ya kugombea Urais katika uchaguzi huu.

Mpayimana alikimbia Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki na ameishi uhamishoni tangu 1994, hasa Ufaransa na Ubelgiji. Mpayimana, ambaye atakuwa akijaribu kwa mara ya pili kumuondoa rais Kagame madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Ana matumaini ya kupata kura kutoka kwa diaspora na anaamini kuwa utulivu wa nchi unategemea kupishana kwa madaraka. Wagombea hao sasa watatembea katika sehemu tofauti za nchi kuwashawishi wapiga kura kuwapa kura zao ifikapo 15 Juali 2024.

Kulingana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Rwanda, watu milioni 9.7 wamejisali kupiga kura katika kinyanganyiro hicho cha kitaifa cha urais na wabunge.

TRT Afrika