Kiwanda kikubwa zaidi Afrika cha kusafisha mafuta na cha kwanza duniani kinachotumia mfumo wa usafishaji wa mashine moja kinazinduliwa Jumatatu na rais anayeondoka wa Nigeria Muhammadu Buhari.
Kiwanda cha Dangote cha kusafisha mafuta ya petroli na kemikali za mafuta kilicho jengwa mjini Lagos ya mtu tajiri zaidi Afrika, Aliko Dangote, kina uwezo wa kusafisha zaidi ya mapipa 650,000 ya mafuta ghafi kwa siku. Baadhi wanabashiri hii kuleta mabadiliko makubwa kwa Nigeria na Majirani zake.
Licha ya kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, Nigeria inategemea zaidi uingizaji wa mafuta iliyosafishwa kutoka nje, kwa matumizi ya ndani, kwa sababu kwa miongo mingi, viwanda vinne vya serikali havikuwa vinafanya kazi vyema.
Hii imesababisha uhaba mkubwa wa mafuta na kuleta kukatika kwa umeme wa mara kwa mara na kupanda ghafla kwa bei.
Kwa mujibu wa benki kuu ya Nigeria, nchi hiyo imetumia zaidi ya $12.44 Bilioni katika kununua mafuta ya nje, 2022 pekee.
Kiwanda cha Dangote kimeahidi kusafisha mafuta ya kutosha kutumiwa nyumbani, hadi kuuza nje.
Katika taarifa kabla ya kuzinduliwa rasmi, kampuni ya Dangote Group, inayomiliki kiwanda hicho ilisema kuwa wameweka ‘matanki 177 yenye uwezo wa kubeba lita bilioni 4.742 ya mafuta.’
Waliongeza kuwa, japo kiwanda hicho kimetengenezwa kwa lengo la kusafisha mafuta ghafi ya Nigeria, kina ‘uwezo wa kusafisha mafuta kutoka kwingine,’ ikiwemo kutoka Mashariki ya Kati na Marekani.
‘‘Tukifikia uzalishaji kamili, tutaweza kutoa 100% ya mahitaji ya bidhaa za mafuta nchini Nigeria na kusalia na kiwango kikubwa cha kuuza nje,’’ kampuni hiyo iliongeza.
Ikiwa na zaidi ya watu milioni 200, Nigeria inahisiwa kutumia zaidi ya lita milioni 60 ya mafuta ya petroli kwa siku kwa mujibu wa maafisa.
Kwa miaka mingi, Nigeria ilizalisha mapipa milioni 200 kwa siku ya mafuta ghafi na uchumi wake unategemea pakubwa mauzo ya bidhaa za mafuta.
Hii ina maana kuwa, mabadiliko yoyote katika sekta ya mafuta, inakuwa na athari fulani katika uchumi wa nchi.
Kiasi kikubwa cha mafuta hayo yanazalishwa maeneo ya kusini ya Niger- Delta, lakini hivi karibuni kumegunduliwa hifadhi za mafuta katika maeneo ya Kaskazini, na uchimbaji unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kiwanda cha kuzalisha kila kitu
Kiwanda hicho cha Dangote kimejengwa katika eneo la soko huru la Lekki mjini Lagos, na kilijengwa katika ardhi kinamasi 'iloyo-okolewa' kwa kujazwa mchanga.
Mwanzoni ilitarajiwa kuwa mradi mdogo lakini baadaye ikapanuliwa na kazi ya ujenzi kuanza mwaka wa 2016.
Majengo hayo yana kiwanda cha kusafisha mafuta, kiwanda cha kemikali na mbolea, yakiwa na bandari yake maalum pamoja na chanzo cha umeme.
Mwanzoni kulikuwa na wasiwasi juu ya mazingira ya uwekezaji, huku baadhi wakitilia shaka hali ya usalama kutokana na mashambulio kutoka kwa makundi yaliyo na silaha hasa dhidi ya viwanda vya mafuta.
Lakini bilionea huyo wa Nigeria, Dangote alipuuza dhana hizo na kuendelea na mradi wake, huku akiamini kuwa kiwanda hicho kitasadisia kuleta usalama katika eneo hilo.
‘Utakapotoa nafasi nyingi za ajira makundi haya yatakosa watu wa kujiunga nao kufanya mashambulio.’ Alijibu Dangote alipoulizwa na wanahabari iwapo ana wasiwasi kuwa ukosefu wa usalama utaathiri mradi wake.
Manufaa nje ya Nigeria
Kampuni hiyo ya Dangote Group inasema kuwa kiwanda hicho kitasafisha mafuta ghafi kutoka Nigeria na kutoka nje pia. Itatarajiwa kuuza nje bidhaa za mafuta ya petroli iliyosafishwa.
Baada ya kiwanda hicho kuanza kazi zake inatarajiwa kupunguza gharama ya mataifa ya Afrika ya kuingiza bidhaa za mafuta kutoka nje ya bara, kulingana na Idakolo Gabriel Gbolade, mtaalamu wa masuala ya uchumi, Nigeria.
Hii ni kwasababu hawata lazimika kuagiza kutoka mbali sana. Hata hivyo haijulikani bado ni lini kiwanda hicho kitaweza kuzalisha kwa asilimia 100, kufikia mapipa 650,000 kwa siku.
Bwana Gbolade, ameaiambia TRT Afrika kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuipatia Nigeria zaidi ya $10Bilioni kwa mwaka, kutoka kwa mauzo ya nje, itakayosaidia nchi kukidhi mapungufu ya biashara zake. Amesema kuwa hii itasaidia kuimarisha sarafu ya Nigeria, Naira.
Kwa mujibu wa msaidizi wa rais Muhammadu Buhari, kampuni ya mafuta ya kitaifa NNPC, imetoa mapipa 300,000 ya mafuta ghafi kwa kiwanda hicho kabla ya kuanza uzalishaji wake ili kuwezesha uzinduzi wa operesheni zake.
Je itapunguza bei ya petroli?
Ujenzi wa kiwanda cha mafuta cha Dangote, kinacho tengeneza pia kemikali kilitarajiwa kuanza 2013 kwa gharama ya $8 Bilioni.
Lakini haukuanza hadi 2016, ambapo ilicheleweshwa zaidi na changamoto za kiuchumi na janga la Uviko-19. Gharama yake pia ilipanda hadi $19 Bilioni kutokana na kubadilika mazingira ya kiuchumi.
Licha ya changamoto hizo, kiwanda hatimaye kimekamilika na hivyo kuongeza matumaini ya kupatikana mafuta kwa wingi zaidi nchini Nigeria.
Rais wa benki ya maendeleo ya Afrika Akinwumi Adeshin, hakuweza kuficha furaha yake alipozuru kiwanda hicho mjini Lagos.
‘Hili ni jukwaa la kibiashara, ambalo linaweza kuisaidia Nigeria na Afrika kwa jumla kupaa zaidi hadi masoko ya kimataifa. Bwana Adeshina aliutaja mradi huo kuwa ‘kampuni ya kuzidisha kasi ya ukuaji Afrika.’
Mtaalamu wa kiuchumi Gbolade pia anatumai kuwa kiwanda hiki kitafungua zaidi ya nafasi 100,000 ya ajira kwa njia moja au nyingine.
Uzinduzi wa kiwanda hiki unakuja wakati Nigeria inapanga kuondoa ruzuku ya mafuta, jambo ambalo litaruhusu nyenzo za soko la mafuta kuathiri kupanda au kushuka kwa bei. Hatua hii imezua hofu ya kupanda mara dufu bei ya mafuta nchini humo.
Hata hivyo mchambuzi Gbolade anaamini kuwa licha ya changamoto hizi, hatimaye kiwanda kikianza uzalishaji kamili, raia wa Nigeria wa kawaida atanufaika pakubwa.