Kenya ndio mwenyekiti wa kamati hii ya Igad iliyoteuliwa kutatua mzozo wa Sudan Picha :Igad

Viongozi wa nchi tano za Mamlaka ya maendeleo ya kiserikali IGAD, wamekutana nchini Ethiopia kwa ajili ya mkutano wa kujadili jinsi ya kuleta suluhu nchini Sudan .

Kenya, Djibouti, Somalia, Sudan Kusini na Ethiopia ziliteuliwa kama kamati ya upatanishi ya Sudan.

Waziri mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia na rais William Ruto wa Kenya walihudhuria mkutano huo.

"Mkutano umeomba kuandaliwa kikao kingine cha marais wanaochangia Kikosi cha Afrika Mashariki ili kufikiria uwezekano wa kutumwa kwa kikosi hiki , kwa ajili ya ulinzi wa raia na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu," taarifa baada ya mkutano huo ulisema.

Viongozi hao wameapa kuzingatia uhuru wa Jamhuri ya Sudan na kuchukua hatua zote za kulinda uadilifu wa nchi hiyo.

Mkutano huo hata hivyo haukuhudhuriwa na majenerali wanaopigana, Abdel Fattah al-Burhan wa jeshi la Sudan na Mohammed Hamdan Dagalo wa kikundi cha Rapid Support Forces.

"Mkutano umesikitishwa na kutokuwepo kwa ujumbe wa Jeshi la Sudan licha ya mwaliko na uthibitisho wa kuhudhuria, " taarifa yake ilisema.

Wakati huo huo wakosoaji wamedai kuwa mkutano huo wa Igad hautafua dafu.

"IGAD itawezaje kutatua vita nchini Sudan ilhali hakuna kiongozi kati yao ameweza kufika mjini Khartoum?" aliuliza Dr. David Matsanga, mtaalamu wa kutatua mizozo.

"Ni lazima kuweza kuongea na majenerali hawa wanaopigana ana kwa ana, na kuwaambia kwamba mambo si mazuri watu wanakufa ovyo," anaongezea.

Kuteuliwa kwa Kenya kama mwenyekiti wa kamati hiyo kulipingwa na kiongoizi wa jeshi la Sudan , jenerali al Burhan. Alidai kuwa rais wa Kenya William Ruto na Kenya wana uhusiano wa karibu na mpinzani wake jenerali Dagalo.

"Changamoto ni kwamba bado majenerali hawa hawajafikia kiwango wanahisi kupata hasara, hadi watakapofika hapo , hawataweza kuweka silaha chini , " Dkt. Edgar Githua , mtaalam wa maswala wa uhusiano wa kimataifa.

Juhudi za Marekani na Saudi Arabia kuwashawishi majenerali hao kusaini makataba wa kusitisha vita mwezi Mei , haujafua dafu kwasababu bado vita vimeendelea.

TRT Afrika