Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa hati ya kukamatwa kwa Edmond Beina, anayeshukiwa kuwa kiongozi wa kundi la wanamgambo.
Beina anatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki, mauaji, ubakaji na mateso, yaliyofanywa katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) mwaka 2014.
Hati hiyo, iliyotolewa mwaka 2018 lakini ikawekwa wazi hivi karibuni, inadai kuwa Beina aliongoza mashambulizi dhidi ya raia wa Kiislamu katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo.
Katika tukio moja maalum, kundi lake linatuhumiwa kuvamia kijiji na kuwaua makumi ya wanaume na wavulana.
Miaka ya vurugu
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa ikikumbwa na ghasia tangu mwaka 2013, wakati wapiganaji wa kundi la Seleka walipomlazimisha Rais wa wakati huo Francois Bozize kuondoka madarakani.
Wanamgambo wanaopinga hilo pia walipigana, na kuwalenga raia na kuwafanya wakazi wengi wa Kiislamu wa mji mkuu, Bangui, kukimbia kwa hofu.
Waendesha mashtaka wanadai kuwa Beina alihusika katika uhalifu katika kijiji cha Guen magharibi mwa nchi hiyo kuanzia Februari hadi Aprili, 2014, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia Waislamu.
Pia aliwaamuru wapiganaji wengine ambao walifanya uhalifu, hii ni kulingana na kibali cha kukamtawa kwake.
Mauaji ya raia
Katika tukio moja, waendesha mashtaka wanadai kuwa Beina na wapiganaji wake walivamia boma la kiongozi wa jumuiya ya Waislamu huko Guen, ambapo takriban watu 300 waliokimbia makazi yao wakiwemo wanawake na watoto walikuwa wamejihifadhi.
"Beina aliwatenganisha raia katika vikundi huku akiwa amewaelekezea bunduki, akawaamuru wanaume na wavulana walale chini.
Kisha, Beina aliwaua wanaume na wavulana kadhaa wa Kiislamu kwa bunduki yake ya Kalashnikov, akiondoa magazine moja na nyingine," kibali hicho kilisema.
"Beina aliamuru watu wake kuwamaliza manusura wowote," iliongeza, ikisema kuwa takriban wanaume na wavulana 42 Waislamu waliuawa katika shambulio hilo.
Watu wengine watatu wanaodaiwa kuwa waasi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sasa wanafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika katika ghasia za kidini nchini humo.