Mwezi Februari, kiongozi mmoja mkubwa ulimwenguni alionya kuwa nchi yake haitosita kutumia silaha za nyuklia iwapo itachokozwa.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa haamini kwamba dunia inaelekea kwenye vita vya nyuklia. Kulingana na Umoja wa Mataifa, Nyuklia ndio “silaha hatari zaidi duniani," kwa wakati huu.
Silaha hizi, ambazo ziko katika mfumo wa mabomu na makombora, zinatumia nishati ya nyuklia kusababisha mlipuko.
Ukubwa wa mlipuko huu unaweza kuathiri masikio, kuharibu ngozi au hata kupofusha macho kutokana na mionzi mikali.
Mlipuko mmoja wa nyuklia una uwezo wa kuteketeza mji mzima ndani ya muda mfupi tu. Mara ya mwisho kutumika kwa silaha hizi ilikuwa ni wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia, ambapo Marekani ilishambulia miji miwili ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan.
Zaidi ya watu 140,000 walipoteza maisha huku asilimia zaidi ya 90 ya makazi zikiharibiwa katika mashambulizi hayo.
Umoja wa Mataifa unakadiria uwepo wa silaha 13,400 za kinyuklia na majaribio 2,000 ya silaha za aina hiyo.
Kutokana na hatari za silaha za nyuklia, mwaka 1946 Umoja wa Mataifa uliunda tume ya kudhibiti matumizi ya silaha hizo wakati wa migogoro ya kijeshi.
Mikataba mitano ya kimataifa dhidi ya matumizi ya silaha za nyuklia imeanzishwa tangu wakati huo, ikiwemo Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia.
Kwa nini silaha za nyuklia ni hatari sana?
Pindi zinapolipuka, silaha za nyuklia hubadilisha mfumo wa kawaida wa hewa na kusababisha joto kali la kufikia nyuzi joto milioni 15, lenye uwezo wa kusababisha majeraha vidonga vikubwa kwenye miili ya binadamu, hata kwa umbali wa kilomita 30.
Wimbi la mlipuko wa Nyuklia huwa na uwezo wa kusafiri maelfu ya kilomita kwa saa.
Athari za muda mrefu ya milipuko ya Nyuklia pia husababisha kuchafuka kwa tabaka la ozoni na hivyo kuwaweka binadamu kwenye hatari zaidi.