Waumini wa Kiislamu wakiwa katika ibada ya  Eid al-Fitr iliyofanyika katika viwanja vya Sir Ali Muslim katika eneo la ngara, mjini Nairobi nchini Kenya / Picha: Reuters

Na

Mazhun Idris

Wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, waumini hutafakari mabadiliko ya ndani yanayotokana na kufunga na kusali.

Eid al-Fitr, siku ya kwanza ya Shawwal au mwezi wa mwandamo unaofuata mzunguko mtakatifu wa Ramadhan katika kalenda ya Kiislamu, ni sherehe ya ushindi huu wa kiroho.

Usomaji wa Quran, ufuasi wa kiibada kwa roho ya iftar na sahur, kufanya matendo mema- kila kitu kinachohusishwa na Ramadhani ni hija ndani.

Sasa, kwa mtazamo wa kwanza wa mwezi mpevu, ni wakati wa safari nyingine. Waislamu wamesimama bega kwa bega tena, mikono yao ikiwa imeinuliwa kwa kuomba dua. Wanatafuta msamaha, mwongozo, na baraka. Nao wanafurahi. Kama wimbo unaofikia kilele chake, Eid al-fitr imewadia.

Mzunguko wa kipekee

Licha ya kwamba Eid huanza asubuhi baada ya siku ya mwisho ya Ramadhan, muda unaweza kutofautiana mara kwa mara kulingana na hesabu za kikanda.

Kwa mwaka 2024, nchi zilizofunga siku 29, kama vile Niger katika Afrika Magharibi, Eid ilidondokea Aprili 9, wakati kwa upande wa nchi zingine, mwezi wa Ramadhan ulikamilisha mzunguko mzima wa siku 30, na Eid kusherehekewa Aprili 10.

Asili ya neno "Eid" ni lugha ya Kiarabu, ambapo maana zake ni pamoja na "sikukuu ya msimu" au "sherehe", inayotokana na neno la msingi la "kurudia" au "kurudi".

Kati ya sherehe mbili kubwa za kila mwaka za Kiislamu, Eid al-Fitr inakuja katika mwezi wa kumi wa kalenda ya Kiislamu.

Sheikh Abdullahi Abatee Abdulsalami, naibu imamu mkuu katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha Uyo katika Jimbo la Akwa Ibom kusini mwa Nigeria, anaelezea Eid al-Fitr kama kipindi cha furaha baada ya safari muhimu ya kiroho.

"Waislamu husherehekea kufanikiwa kwa wajibu wa kimungu wa mfungo wa mwezi mzima, nguzo ya imani yao. Kuaga mwezi mtukufu wa kujiepusha na chakula na starehe kuanzia alfajiri hadi kuchwa kwa jua kunaitaka karamu ya kufurahia mafanikio haya ya kiroho." anaiambia TRT Afrika.

Wakiwa wamevalia vyema kwa ajili ya sherehe hiyo, Waislamu huenda msikitini au uwanjani kuswali siku ya Eid kinayoongozwa na imamu wa jumuiya.

Baada ya hapo, sherehe hizo huambatana na ndugu kutembeleana, kukaa pamoja kulingana na tamaduni zao.

Ugumu wa maisha

Japokuwa si wote hubahatika kufurahi na familia zao katika sikukuu hii, Nezeef Ahmed, mkazi Abuja, anaamini kuwa Eid ni zaidi ya sherehe ya kawaida.

"Eid imekuja kipindi kigumu kiuchumi, lakini kama ilivyo ada, tunamshukuru Mungu kwa kila jambo," anaimbia TRT Afrika.

"Tunasherehekea licha ya changamoto zote. Baada ya kuwapeleka watoto wangu wawili kwenye swala ya Eid asubuhi, nitarudi nyumbani kuwaandalia chakula wageni ninaowatarajia. Watu watasherehekea, kucheza na kucheka licha ya magumu."

Lakini Eid ni zaidi ya kushiba baada ya muda wa kujizuia.

"Roho ya kutoa na kushiriki inawakilishwa na sikukuu hii," anasema Sheikh Abdulsalami. "Kadiri unavyoshiriki zaidi, ndivyo furaha inavyokuwa kubwa."

Familia nyingi husafiri kwenda mijini au nchi walizozaliwa ili kusherehekea pamoja na familia na jamaa.

Kama ilivyo kwa mambo yote yanayofungamana na utamaduni na imani, Eid al-Fitr inasalia kuwa muunganiko wa kila kitu.

Eid Mubarak!

TRT Afrika