Na Coletta Wanjohi
Kila siku asubuhi, kwenye kipindi chake cha redio, Salma Msangi anazungumza kuhusu masuala yanayohusu uzazi, akijitoa kama mfano kwa uzoefu wake binafsi wa kulea mtoto.
Wasikilizaji nchini Tanzania wanaofuata kipindi chake wanafahamu maoni yake kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee, ambayo anaitetea kwa dhati.
"Nilipojifungua mwanangu wa kwanza, nilikumbana na changamoto katika kunyonyesha," Salma anasimulia TRT Afrika.
Akiwa mama mchanga, alijawa na mashaka wakati familia na marafiki walipomwambia kwamba alikuwa akimnyima mtoto lishe ya kutosha kwa kutegemea maziwa ya mama pekee.
“Ilinilazimu kutafuta msaada kutoka hospitali nilikojifungua,” anasema. "Wataalamu wa matibabu walinipa mafuzno sana, na kunifanya kutambua kuwa maziwa ya mama yanatosha kwa mtoto angalau katika miezi sita ya kwanza."
Lakini hili si jambo la mjini tu.
Katika kijiji kimoja Magharibi mwa Kenya, Sarah Khatievi anafurahia kuwa pamoja na wajukuu zake sita ambao wamekuja kumtembelea.
Sarah mwenye umri wa miaka 68 anaiambia TRT Afrika kwamba watoto wake wote wanane, aliwapa maziwa ya matiti, lakini pia pole pole akaongeza chakula kingine.
"Mtoto hawezi kushiba na maziwa ya mama pekee - hivyo ndivyo mama zetu walitufundisha," anasema Sarah.
"Kwa watoto wangu wote, ningeongeza maji kwenye lishe pamoja na maziwa ya mama. Takriban miezi mitano, nilianzisha viazi vilivyopondwa kuwa rojo, na polepole nikaongeza uji nyepesi, kabla ya kuanza kuwapa chakula kabisa baada ya miezi sita," anaongeza.
Sarah anacheka sana hadithi ambazo anasema zilihusishwa na kumlea mtoto wakati wa zamani.
Mama yake alimwambia kwamba ili mtu ajue kwamba mtoto ameshiba, ujanja ni kuendelea kuangalia ukubwa wa tumbo wakati mtoto anakula.
"Tumbo linapopata umbo wa mpira basi unajua mtoto wako ameshiba, "
Lishe ya kipekee
Kumlisha mtoto kwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita tangu kuzaliwa inashauriwa kama lishe bora ya kipekee na wataalam wa afya.
Wanashauri pia kuwa mama aanzishe kunyonyesha ndani ya saa moja baada ya mtoto kuzaliwa, ingawa hilo linathibitisha changamoto kwa wanawake wengi.
"Baadhi ya akina mama wana wasiwasi wa kukosa maziwa ya kutosha kwa watoto wao," anasema Victoria Kirway, muuguzi aliyebobea katika huduma ya watoto wachanga katika Hospitali ya CCBRT katika jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania.
"Siku zote tunasema kwamba kunaweza kuwa na matatizo kwa sababu ya mabadiliko ya homoni, lakini hatimaye maziwa ya mama yatazalishwa kwa kawaida."
Victoria anasema mama hahitaji kuwa na wasiwasi juu ya kutoa maziwa ya mama ya kutosha, akihakikishia kwamba yatatokea tu kwa kawaida,
“Mtoto anapozaliwa, hahitaji maziwa mengi: hivyo, yale mtoto anapata kwa matiti ya mama yanatosha. Mama anafaa amuweke mtoto kwa matiti anyonye kila baada ya saa mbili au tatu, na maziwa ya mama yataendelea kuongezeka."
Mtindo wa urembo
“Unasikiliza kutoka wapi? Niambie kwa nini hunyonyeshi," Salma anasikika akisema katika sehemu ya pili ya kipindi chake cha redio, na mara tu anawawekea wasikilizaji wake wimbo maarufu wa kiswahili unaoongelea wasichanna warembo
Sehemu hii ya kipindi chake ni maarufu na huvutia wasikilizaji wengi wanaopiga simu hasa wasichana ambao huzungumza waziwazi vile kunyonyesha kutawafanya waharibu urembo wao.
"Watu daima wanataka kuzungumzia swala hili, ni mada ambayo haizeeki," Salma anaiambia TRT Afrika.
“Wanawake wengi walio bado vijana wanaamini kwamba wakinyonyesha, ukubwa na umbo la matiti yao itaathirika,” anasema mama huyo wa watoto watatu.
"Wanawake wenzangu hawaelewi kwamba umbo na ujazo wa matiti yetu yanatawaliwa na maumbile, sio kunyonyesha."
Mashirika ya WHO na UNICEF yanasema kuwa "watoto ambao hawanyonyeshwi wana uwezekano mara 14 zaidi wa kufa kabla ya kufikia mwaka mmoja wakilinganishwa na wale wanaonyonyeshwa kwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza".
"Tuna akina mama wanaokuja na watoto wagonjwa na tunapouliza, wanatuambia watoto hawajawahi kunyonyeshwa. Mara nyingi inatokea kwamba akina mama hao hawana sababu za kiafya za kutowapa watoto wao maziwa ya mama," Anasema nesi Victoria.
''Wataalamu wanashauri mama kujizuia kumnyonyesha mwanaye, iwapo ana virusi vya HIV ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa mama hadi mtoto - jambo ambalo mzazi anapata ushauri zaidi wakati wa uja uzito.''
Kulingana na madaktari, mtoto ambaye amenyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza baada ya kuzaliwa huwa na kiwango cha juu cha akili.
"Siku zote tunawaambia akina mama hawa kuwa wakiwanyima watoto wao maziwa ya mama wanajenga utamaduni wa watoto wao kuwa na kinga ndogo dhidi ya magonjwa, " Victoria aneleza TRT Afrika
"Unyonyeshaji ni jambo lisilo gumu na unaweza kumuepusha mtoto na homa ya mapafu, homa ya uti wa mgongo, magonjwa ya mishipa ya mkojo, pumu, kisukari, matattizo ya unene ya kupita kiasi na matatizo ya moyo. ,” anasema Victoria.
Kunyonyesha pia kunamuokoa mtoto kutoka kwa vifo vya ghafla vya watoto hasa wakiwa usingizini.
Lakini pia ina manufaa kwa akina mama.
Shirika la WHO linasema kuwa inawakinga akina mama dhidi ya saratani ya matiti na ovari.
WHO inasema baadhi ya nchi barani Afrika kama Côte d'Ivoire na Somalia zimeonyesha juhudi ya ongezeko la viwango vya kuwasaidia akina mama kuongeza unyonyeshaji hasa kutokana na kampeni kuhusu faida zake.
Kunyonyesha na kufanya kazi
Matarajio ya mama kurudi tena kazini baada ya kujifungua, na ukosefu wa mazingira ya kunyonyesha katika maeneo ya kazi ni changamoto kwa akina mama ambao wangependa kuendelea kuwanyonyesha watoto wao kwa miezi sita.
Dunia inapoadhimisha wiki ya kunyonyesha, Agosti 1 hadi 7 , mashirika ya WHO na UNICEF yametangaza kauli mbiu ya mwaka huu kuwa : Fursa ya kunyonyesha ukiwa kazini.
Mashirika haya yamehimiza waajiri wote kuunga mkono unyonyeshaji mahali pa kazi,
"Kutoa likizo ya malipo ya kutosha kwa wazazi na walezi wote wanaofanya kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto wao wachanga ni muhimu pia, Hii inajumuisha likizo ya uzazi yenye malipo kwa angalau wiki 18, ikiwezekana kwa muda wa miezi sita au zaidi baada ya kuzaliwa, " zimesema katika taarifa.