Mahatma Gandhi, kiongozi wa zamani wa kisiasa na kiroho nchini India./Picha: Getty

Ulimwengu unaendelea kushuhudia machafuko yanayoendelea kupoteza uhai wa watu wengi kila kukicha.

Kwa mfano, hadi kufikia Oktoba 2, 2024, jumla ya Wapalestina 41, 615 wameuwawa na majeshi ya Israeli, tangu kuanza kwa machafuko hayo, Oktoba 7 mwaka 2023.

Kama hiyo haitoshi, mashambulizi ya hivi karibuni nchini Lebanon tangu Septemba 23 zaidi ya 800 wamepoteza maisha tangu kufuatia mashambulizi ya Israeli nchini Lebanon.

Alama ya kupinga machafuko kama inayoonekana nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, nchini Marekani./Picha: Getty

Hata hivyo, dunia bado inaendelea kuwakumbuka baadhi ya watu waliokuwa mstari wa mbele kueneza itikadi na falsafa zao bila ya kutumia vurugu na machafuko.

Watu hao walitumia njia tofauti za kupigania haki zao na haki za wengine, na hata kutaka fikra zao zitambulike bila kutumia aina yoyote ya nguvu wala machafuko.

Mahatma Gandhi

Huyu alikuwa ni kiongozi wa harakati za uhuru wa India. Mahatma, ambaye jina lake halisi ni Mohandas Karamchand Gandhi, aliamini katika maendeleo ya watu, heshima na haki, uhuru wa kuabudu na haki sawa kwa wote.

Katika vuguvugu lake la kudai uhuru toka kwa Waingereza, Mahatma Gandhi hakuamini wala hakutumia fujo na nguvu dhidi ya binadamu mwengine. Aliuwawa Januari 30, 1948.

Mahatma Gandhi, ambaye jina lake halisi ni Mohandas Karamchand Gandhi, aliamini katika maendeleo ya watu, heshima na haki, uhuru wa kuabudu na haki sawa kwa wote./Picha: Getty

Desmond Tutu

Askofu huyo wa zamani wa kanisa la Kiinglikana la nchini Afrika Kusini alikuwa mpigania uhuru wa kikanisa dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Mshindi huyo wa tuzo ya Amani ya Nobel, alilaani matumizi ya nguvu na hakuwahi kutetea maandamano yoyote yaliyo tawaliwa na vurugu, kwani alikuwa muumini wa kudai haki kwa njia za amani.

Mshindi wa zamani wa tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu./Picha: Getty

Sifa hiyo ilimpa Askofu Tutu uenyekiti wa Tume ya Ukweli na Maridhiano ya nchini Afrika Kusini.

“Usipaze sauti yako, boresha hoja yako,” aliwahi kusema Askofu huyo.

Martin Luther King, Jr.

Martin Luther King, Jr. wa Marekani akiwahutubia wafuasi wake./Picha: Getty

Martin Luther King, Jr. atakumbukwa kwa mafanikio yake ya kutetea na kupigania haki za kiraia nchini Marekani.

Lakini kwa kipekee zaidi, ni mbinu alizotumia wakati wa kudai haki hizo.

Martin Luther King Jr alikuwa kiongozi wa "The Southern Christian Churches Leadership", likifanya kazi kubwa ya kuratibu makanisa ya watu weusi na kuandaa harakati za kupinga ubaguzi bila kutumia nguvu au vurugu.

Mwaka 1964 alishinda tuzo ya Nobel kutokana na harakati zake za kutetea usawa kwa weusi bila matumizi ya vurumai, lakini pia alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakipinga sana vita ya Vietnam.

Atakumbukwa sana hasa katika hotuba yake maarufu ya "I HAVE A DREAM" Akimaanisha "Nina ndoto" ambayo ilitoa unabii mkubwa sana wa Uhuru, haki na Usawa na hatimaye Dunia ilishuhudia Marekani ikiongozwa na Mmarekani mweusi, Barack Obama wakati miaka ya nyuma ilikuwa ni marufuku kwa wamarekani weusi kushiriki katika medani za kisiasa na hata kupiga kura.

Dalai Lama

Dalai Lama./Picha: Getty

Dalai Lama, kiongozi wa kiroho wa Tibet, aliwahi kuandika ujumbe wa kupinga machafuko na kudumisha huruma wakati wa kutafuta suluhu ya migogoro duniani.

Alifanya kitendo hiko wakati wa kuadhimisha miaka 75 ya kupitishwa kwa Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu.

Mara kwa mara, kiongozi huyo wa kiroho amekuwa akionesha hamu ya kuona mabadiliko katika ulimwengu kwa kuchagua njia isiyo ya vurugu ya kusuluhisha mizozo kwa amani, kwa msingi wa mazungumzo.

TRT Afrika