Dunia ina jukumu la kuzuia mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel - Ramaphosa

Dunia ina jukumu la kuzuia mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel - Ramaphosa

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema nchi yake ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mzozo wa Gaza.
Rais Cyril Ramaphosa amesema nchi yake inaelewa thamani ya uungaji mkono wa kimataifa kwa haki ya watu kujitawala na utaifa/ Picha: AFP

Akizungumza katika mkutano wa 16 wa wakuu wa nchi za BRICS, Rais wa Afrika Kusina Cyril Ramaphosa alisema, "Nchi za dunia zina jukumu la kutofadhili au kuwezesha vitendo vya mauaji ya halaiki ya Israel.''

BRICS ni kundi la nchi zinazoibukia ambazo ni pamoja na Brazil, Urusi, India, China, na Afrika Kusini, pamoja na Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

"Kama Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeamua sasa, nchi za ulimwengu zina jukumu la kukuza utambuzi wa haki ya watu wa Palestina ya kujitawala," alisema.

Ramaphosa alisema nchi yake ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka zaidi kwa mzozo ambao tayari umesababisha vifo na uharibifu mkubwa.

BRICS ni kundi la nchi zinazoibukia ambazo ni pamoja na Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini, pamoja na Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu/ Picha: Ofisi ya waziri Mkuu Ethiopia

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alisema nchi yake inaelewa thamani ya uungaji mkono wa kimataifa kwa haki ya watu kujitawala na utaifa, kutokana na historia yake ya ubaguzi wa rangi.

Kesi huko katika mahakama ya ICJ

Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika Mahakama ya ICJ iliyoko The Hague mwishoni mwa 2023, ikiishutumu Israel, ambayo imeshambulia kwa bomu Gaza tangu Oktoba mwaka jana, kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya 1948.

Mwezi Mei, ICJ iliiamuru Israel kusitisha mashambulizi yake katika mji wa kusini wa Gaza wa Rafah. Ilikuwa ni mara ya tatu kwa jopo la majaji 15 kutoa maagizo ya awali ya kutaka kudhibiti idadi ya vifo na kupunguza mateso ya kibinadamu katika eneo lililozingirwa, ambapo idadi ya majeruhi imevuka 44,000.

Ramaphosa alisema amani na usalama wa kudumu hautapatikana hadi pale Wapalestina watakapotimiza matarajio yao ya kuwa taifa, haki na uhuru.

"Amani na usalama duniani kote unahitaji utashi wa pamoja wa jumuiya ya mataifa. Unahitaji Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo ni mwakilishi na shirikishi,” alisema.

Ramaphosa alisema wanaona mizozo mingi ikiendelea duniani kote, na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijatimiza wajibu wake wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

"Haiwakilishi maslahi ya jumuiya ya kimataifa, na kwa hivyo haina njia ya kutekeleza tamaa ya kimataifa ya amani."

Alisema kama vile BRICS ina jukumu muhimu katika kuunda mpangilio mpya wa ulimwengu wa pande nyingi, vivyo hivyo lazima itumie sauti yake kuendeleza mabadiliko.

"Tulipata makubaliano juu ya mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tulipokutana Johannesburg mwaka jana," Ramaphosa alisema, akirejea mkutano wa kilele wa BRICS uliofanyika Afrika Kusini mwaka jana.

TRT Afrika