Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Brics wanakutana nchini Afrika Kusini kwa mazungumzo ambayo ni utangulizi wa mkutano mkubwa wa viongozi wa nchi zinazoendelea unaotarajiwa kufanyika Agosti mjini Johannesburg.
Rais wa Urusi Vladimir Putin ni miongoni mwa viongozi - akiwemo Xi Jinping wa China - ambao wamealikwa katika mkutano huo, ingawa utata unazingira uwezekano wa kuhudhuria kwake baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutoa hati ya kukamatwa kwake kwa madai ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.
Afrika Kusini ilithibitisha kuwa mawaziri wa mambo ya nje kutoka Brazil, Urusi, India na Afrika Kusini wanahudhuria mkutano wa Alhamisi mjini Cape Town. Naibu waziri anaiwakilisha China.
Brics ni kundi linaloleta pamoja nchi zinazoendelea kiuchumi zinazoundwa na Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Hakuna ajenda ambayo imetolewa kwa umma kuhusu mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje, lakini wachambuzi walisema majadiliano yatazingatia upanuzi wa kundi hilo na kuunda sarafu ya Brics, mashirika ya habari yanaripoti.
Hatua hizo zinaweza kutoa uzani dhidi ya utawala wa kijiografia wa Magharibi.
Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Venezuela, Argentina, Iran na Algeria wanasemekana kuwa katika orodha ya wanaotaka kujiunga na umoja huo, kwa mujibu wa maafisa.
"Kama wanaweza kuleta nchi zinazozalisha mafuta ambazo zitakuwa muhimu, kutokana na mfumo wa petroli," William Gumede, mchambuzi wa kisiasa wa Afrika Kusini, alinukuliwa akisema na shirika la habari la Reuters.
Rais wa Brazil Lula da Silva mwezi uliopita alitoa wito kwa mataifa ya Brics kupitisha sarafu ya pamoja ili kusaidia kuongeza biashara na uwekezaji miongoni mwa nchi wanachama. Majadiliano ya hapo awali juu ya sarafu ya pamoja hayajazaa matunda.
Mkutano wa Brics unakuja kufuatia mkutano wa kilele wa Kundi la Viongozi Saba nchini Japan ambao ulitawaliwa na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na kukabiliana na ushawishi wa China.