Viongozi wa dunia wametoa wito wa kutaka kuwepo kwa amani Mashariki ya Kati na Ukraine katika mkutano wa viongozi wa nchi za BRICS nchini Urusi siku ya Jumatano, huku Rais Vladimir Putin akiwaambia kuwa anakaribisha wazo la upatanishi katika mzozo wa Ukraine.
Kiongozi wa Urusi anatoa kauli hiyo katika mkutano huo kama ishara ya kuonyesha kwamba majaribio ya Magharibi ya kuitenga Moscow yameshindwa, lakini alikabiliwa na wito wa moja kwa moja wa kumaliza mzozo wa Ukraine kutoka kwa washirika wake wa karibu na muhimu zaidi.
Mkutano wa viongozi wa dunia wapatao 20 katika mji wa kati wa Kazan ndio kongamano kubwa zaidi la kidiplomasia nchini Urusi tangu "operesheni maalum ya kijeshi" ya nchi hiyo nchini Ukraine mnamo 2022.
Kuanzia mwaka 2009 ikiwa na wanachama wanne - Brazil, Russia, India na China - BRICS imepanuka na kujumuisha mataifa mengine kama vile Afrika Kusini, Misri na Iran.
Rais wa China Xi Jinping aliuambia mkutano huo kwamba lazima "mapigano yasiongezeke" nchini Ukraine.
"Lazima tuzingatie kanuni tatu za 'kutokimbia kutoka uwanja wa vita, hakuna kuongezeka kwa mapigano na kutoongeza mafuta kwenye moto kwa pande husika,' ili kurahisisha hali haraka iwezekanavyo," Xi alisema.
Urusi na Uchina zilitia saini makubaliano ya kimkakati ya "bila kikomo" yaani : no limits" siku chache kabla ya Moscow kuamuru wanajeshi kuingia Ukraine na Putin na Xi wote walipongeza uhusiano wa karibu katika mkutano wa pande mbili mnamo Jumanne.
Bila kutaja mzozo wowote maalumu, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia alitoa wito wa amani.
"Tunaunga mkono mazungumzo na diplomasia, sio vita," alisema.
Matoleo ya upatanishi
Kuhusu Mashariki ya Kati, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian aliwataka wanachama wa BRICS "kutumia uwezo wao wote wa pamoja na mtu binafsi kumaliza vita huko Gaza na Lebanon".
Xi alirudia wito wake wa kusitishwa kwa mapigano, akisema, "Tunahitaji... kukomesha mauaji na kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya suluhu ya kina, ya haki na ya kudumu kuhusu suala la Palestina."
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva pia alitoa wito wa kutaka kuepukwa kwa kuongezeka kwa vita Mashariki ya Kati na Ukraine.
"Tunapokabiliana na vita viwili ambavyo vina uwezo wa kuwa vya kimataifa, ni muhimu kurejesha uwezo wetu wa kufanya kazi pamoja kwa malengo ya kawaida," alisema katika hotuba yake kwenye mkutano huo kupitia mkutano wa video.
Katika mazungumzo ya faragha, Putin alikaribisha pendekezo kutoka kwa viongozi kadhaa wa BRICS kufanya upatanishi nchini Ukraine, hata kama aliwaambia majeshi yake yanasonga mbele, msemaji wake alisema Jumatano.
Nchi nyingi "zilielezea nia ya kuchangia kikamilifu" katika kutatua mzozo huo, vyombo vya habari vya serikali vilimtaja msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov akiwaambia waandishi wa habari.
Putin pia ametumia mikutano hiyo kupigia debe "mienendo chanya ya mbele kwa vikosi vya jeshi la Urusi," Peskov alisema.
Wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisogea polepole mashariki mwa Ukraine kwa muda mrefu wa 2024, ingawa hakuna upande ambao umeweza kupata mafanikio makubwa katika mzozo unaonekana kuwa katika hatua ya mwisho.
"Kuepuka vita na kuanzisha mazungumzo ya amani pia ni muhimu katika mzozo kati ya Ukraine na Urusi," Lula wa Brazil alisema.
Utaratibu wa amani duniani
Xi na Modi hapo awali walipendekeza mipango yao ya amani kwa Ukraine, ingawa kumeonekana kuwa na maendeleo kidogo.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, pia yupo katika mkutano huo, aliwasili Urusi siku ya Jumatano, mashirika ya habari ya serikali ya Urusi yaliripoti.
Atafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Putin baadaye siku ya Jumatano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alikuwa kwenye mkutano huo, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini Urusi kwa zaidi ya miaka miwili.
Atafanya mazungumzo na Putin kuhusu Ukraine siku ya Alhamisi.
Moscow inakuza jukwaa la BRICS kama mbadala kwa mashirika ya kimataifa yanayoongozwa na Magharibi kama vile G7.
"Mchakato wa kuunda mpangilio wa ulimwengu wa pande nyingi unaendelea, mchakato wenye nguvu na usioweza kutenguliwa," Putin alisema katika ufunguzi rasmi wa mkutano huo.
Pia alikashifu nchi za Magharibi kwa kuwawekea vikwazo wanachama wa BRICS, ikiwa ni pamoja na Urusi, akisema vinaweza kusababisha mzozo wa kimataifa.
"Uwezo mkubwa wa mgogoro pia upo. Na sio tu kuhusu mvutano wa kijiografia unaoendelea kuongezeka, lakini pia ... desturi ya vikwazo vya upande mmoja, ulinzi na ushindani usio wa haki unapanuka," Putin alisema.
Putin pia alitoa wito kwa viongozi wa nchi zinazoinukia kiuchumi kuchunguza malipo mbadala na majukwaa ya biashara ili kupunguza utegemezi wao wa miundombinu ya Magharibi.