Watu11 walikufa katika ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kulipuka Oktoba 22, 2024 Uganda/ Picha: Reuters

Spika wa Bunge la Uganda Anitah Among ametoa wito wa raia kuhamasishwa zaidi juu usalama.

Hii inafuatia ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kulipuka saa tisa mchana, Oktoba 22, 2024 .

Ajali ilitokea katika mji wa Kigogwa pembezoni mwa barabara ya Kampala-Bombo huko Kasangati, Wilaya ya Wakiso na kusababisha kifo na majeraha. Watu 9 na watoto 2 wanaripotiwa kuunguzwa bila kutambuliwa.

"Lori hilo la mafuta, lenye namba za usajili UAM 292Q, lilikuwa likisafiri kutoka Kampala kwenda Gulu wakati ajali hiyo ilipotokea. Kwa bahati mbaya, watu waliokimbia kuchota mafuta ndio walioathirika zaidi," Polisi Uganda ilisema katika akaunti yake ya X.

Utambulisho wa walioathirika bado haujawekwa wazi / Picha: Reuters 

Spika wa Bunge Among ametoa rai hiyo Jumatano wakati wa kikao cha mashauriano ambapo aliliongoza Bunge kwa kutoa pole kwa familia za watu 11 waliofariki katika ajali hiyo.

"Katika miaka michache iliyopita, tumeshuhudia kesi kama hizo hasa Januari 2021 ambapo zaidi ya watu 33 walikufa. Huko Rubirizi mnamo 2019, watu 20 walikufa. Matukio kama haya yanaonyesha hitaji la kuhamasisha wenyeji wetu juu ya usalama wa umma wakati wa matukio kama haya," Among alisema katika kikao cha bunge.

Nae mbunge Naluyima Ethel anasema idadi ya watu waliofariki kutokana na tukio hilo la moto inazidi kuongezeka.

Amependekeza kwamba ni wakati muafaka wa kusambaza huduma ya uokoaji wa vikosi vya zimamoto katika maeneo yenye shughuli nyingi nchini, kwa sababu wengi waliathirika kutokana na kuchelewa kufika kwa kikosi cha zimamoto.

Majeruhi walikimbizwa katika vituo vya afya vilivyo karibu kwa matibabu na polisi inasema inafanya uchunguzi kutoka vituo vya afya kuthibitisha idadi ya watu waliojeruhiwa.

"Tukio hili la kusikitisha ni ukumbusho wa hatari zinazohusiana na ajali za malori ya mafuta na umuhimu wa kuwa waangalifu wakati wa kushughulikia vifaa hatari," Polisi imeongezea ikisema itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo na walioathiriwa.

Utambulisho wa walioathirika bado haujawekwa wazi.

TRT Afrika