Sudan / Photo: AFP

Vikosi vya kijeshi vya Urusi vilisema Jumanne vinawahamisha zaidi ya watu 200 kutoka Sudan kwa ndege nne za kijeshi za usafiri.

Wizara ya ulinzi ilisema katika taarifa yake waliohamishwa ni pamoja na wanadiplomasia, wanajeshi na raia wengine wa Urusi pamoja na raia wa "nchi za uliokuwa Muungano wa Sovieti na nchi nyingine rafiki ambao waliomba msaada".

Ndege iliyobeba kundi la mwisho la wakimbizi wa Uingereza pia iliondoka Sudan Jumatatu jioni huku nchi kadhaa zikiendelea kuwarejesha makwao raia wao kutoka nchini humo.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths anatarajiwa nchini Sudan kusaidia katika utatuzi wa kidiplomasia wa mzozo huo.

Alitumwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye aliitaja hali katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini ''haijawahi kushuhudiwa.''

Mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 500, maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha kuhama kwa wageni na wafanyikazi wa kimataifa.

Umoja wa Mataifa unasema unatazamia watu wapatao 800,000 kutoroka Sudan kama wakimbizi huku ghasia zikiendelea.

Mzozo huo ni kati ya vikosi vya jenerali wa jeshi Abdel Fattah al-Burh an na makamu wake wa zamani, Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi.

TRT Afrika na mashirika ya habari