Rais Hakainde Hichilema siku ya Jumanne amehudhuria hafla ya kuadhimisha miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa kampuni ya sukari ya Zambia Sugar PLC, na kuipongeza kampuni hiyo kwa kufikia hatua hii muhimu.
Kama mojawapo ya wazalishaji wakuu wa sukari barani Afrika, Zambia Sugar imekuwa kinara wa uwekezaji, ukuaji, na uundaji wa nafasi za kazi, ikichangia uchumi wa nchi na kuathiri masoko ya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Hichilema aliangazia uwiano kati ya mafanikio ya Zambia Sugar na Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa taifa hilo, akiweka kampuni hiyo kama kielelezo cha mafanikio ya kuigwa na sekta nyinginezo.
Kupitia mtandao wa 'X', Rais Hakainade Hichilema amepongeza juhudi za kampuni hiyo kwa kuwezesha wakulima wengi wadogo na kuunda ajira.
Alisisitiza umuhimu wa mpango wa wakulima wa nje wa kampuni, ambao umewawezesha wakulima wengi wadogo karibu na enelo la Mazabuka, na kuhimiza kuendelea kwa upanuzi wa mpango huo ili kuwanufaisha wakulima wengi zaidi.
Kwa kuzingatia changamoto za nishati zinazoendelea nchini humo, zikiwa mbaya zaidi kutokana na hali ya ukame, Rais aliipongeza Zambia Sugar kwa mbinu yake ya ubunifu katika uzalishaji wa nishati.
Kampuni hiyo kwa sasa inazalisha megawati 40 za umeme na inajitahidi kuongeza uwezo kwa megawati 60 za ziada, ambazo zitaleta jumla ya uzalishaji wao hadi megawati 100, ambao itatosha kuchangia nishati ya ziada kwenye gridi ya taifa kupitia ZESCO.