Mamlaka nchini Congo ilisema iliwaachilia wafungwa 600 katika gereza kuu la nchi hiyo siku ya Jumamosi kama sehemu ya mchakato unaolenga kupunguza msongamano wa magereza.
Waziri wa Sheria Constant Mutamba alitangaza hatua hiyo wakati wa hafla katika Gereza Kuu la Makala katika mji mkuu wa Congo, Kinshasha.
''Kuna mipango ya ujenzi wa gereza jipya huko Kinshasa,'' alisema Mutamba, bila kutoa maelezo zaidi.
Gereza la Makala, gereza kubwa zaidi nchini Kongo lenye uwezo wa kuchukua watu 1,500, linawashikilia zaidi ya wafungwa 12,000, wengi wao wakisubiri kesi zao kusikizwa, Amnesty International ilisema katika ripoti yake ya hivi punde ya nchi.
Mapema mwezi huu, jaribio la wafungwa kutoroka katika gereza hilo lilisababisha vifo vya watu 129, wakiwemo wengine waliopigwa risasi na walinzi na askari na wengine waliofariki katika mkanyagano katika kituo hicho kilichojaa watu, kulingana na mamlaka.
Emmanuel Adu Cole, mwanaharakati mashuhuri wa haki za magereza nchini Congo, alidai kuwa huenda idadi hhiyo imefika zaidi ya 200.
Hali mbaya na madai ya unyanyasaji
Pia kulikuwa na visa kadhaa vya wanawake kubakwa wakati wa jaribio hilo lakutoroka jela, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Congo Jacquemin Shabani alichapisha kwenye X mapema mwezi huu, bila kufafanua.
Wafungwa walikuwa wamezidi kulalamikia hali mbaya katika kituo hicho, ikiwa ni pamoja na vitanda duni, lishe duni na usafi wa mazingira.
Hata hivyo, mamlaka ilishindwa kuchukua hatua licha ya onyo, alisema Cole, ambaye msingi wake umetembelea gereza hilo hapo awali.
"Tumekuwa na wakati mgumu katika siku za hivi karibuni kwa kila kitu kilichokuwa kikitokea hapa, kulikuwa na ubakaji, tulikuwa waathirika, wengi wetu walikufa," alisema Prisca Mbombo, mmoja wa wafungwa walioachiliwa.
Stanis Bujakera Tshiamala, mwandishi wa habari mashuhuri wa Kongo ambaye hivi majuzi alizuiliwa katika gereza hilo kwa miezi kadhaa, alizungumzia hali yake "ya kusikitisha na ya kinyama" na jinsi wafungwa mara kwa mara wanakosa chakula, maji na huduma za matibabu.
Takriban wanawake 700, na mamia ya watoto wadogo ambao "wanatendewa sawa na watu wazima," ni miongoni mwa wafungwa, alisema.