Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni miongoni mwa nchi kumi duniani ambazo zina idadi kubwa ya watoto ambao hawajapata chanjo ya kwanza ya surua.
Nchi hizo mbili, hata hivyo, zimesajili "maendeleo makubwa" katika chanjo, WHO imesema, lakini bado zinahitaji juhudi zaidi.
Nchi nyengine za Afrika ambazo zimepiga hatua kubwa katika ufuatiliaji wa chanjo dhidi ya surua ni Sudan Kusini, Cameroon, Malawi na Msumbiji.
Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan zitaanza kampeni kubwa ya chanjo kabla ya mwisho wa 2024, WHO imesema katika taarifa yake ya Alhamisi.
Shirika la WHO linasema kuwa kati ya watoto milioni 22 ambao walikosa kipimo chao cha kwanza cha chanjo ya surua mwaka 2022, zaidi ya nusu wanaishi katika nchi 10 pekee.
Hizi ni pamoja na Angola, Brazili, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, , Madagascar na Nigeria.
Surua au Measles ni nini?
Surua, ambayo ni mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo vya watoto wadogo, husababishwa na virusi, na kwa kawaida hupitishwa kupitia mguso wa moja kwa moja na kupitia hewa.
Surua ni ugonjwa unaoambukiza sana unaosababishwa na virusi. Huenea kwa urahisi wakati mtu aliyeambukizwa anapopumua, kukohoa au kupiga chafya.
Dalili za surua kawaida huanza siku 10-14 baada ya kuambukizwa virusi.
Upele ni dalili inayoonekana zaidi.
Inaweza kusababisha ugonjwa mbaya, matatizo na hata kifo.
Surua inaweza kuathiri mtu yeyote lakini ni kawaida zaidi kwa watoto.
Surua huathiri njia ya upumuaji na kisha kusambaa katika mwili wote. Dalili ni pamoja na homa kali, kikohozi, mafua na upele mwili mzima.
Chanjo ya surua
Surua inaweza kuzuilika kwa dozi mbili za chanjo.
Chanjo ya jamii nzima ndiyo njia bora zaidi ya kuzuia surua. Watoto wote ni muhimu kupewa chanjo dhidi ya surua.
Watoto wanafaa kupokea dozi mbili za chanjo, dozi ya kwanza kwa kawaida hutolewa katika umri wa miezi 9 katika nchi ambazo surua ni ya kawaida miezi 12-15 katika nchi nyingine.
Dozi ya pili kutolewa baadaye utotoni, kwa kawaida katika miezi 15-18.
Kuchanjwa ni njia bora ya kuzuia kuugua surua au kueneza kwa watu wengine. Chanjo ni salama na husaidia mwili wako kupambana na virusi.