Kesi mahakamani ya daktari wa Rwanda anayetuhumiwa kwa mauaji ya halaiki ilifunguliwa mjini Paris siku ya Jumanne, miongo mitatu baada ya mauaji ya Watutsi wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Eugene Rwamucyo, 65, anatuhumiwa kusaidia mamlaka ya nchi yake katika kueneza propaganda dhidi ya Watutsi na kushiriki katika mauaji ya halaiki katika jaribio la kuharibu ushahidi wa mauaji ya halaiki.
Daktari huyo ambaye alifanya kazi ya udaktari nchini Ufaransa na Ubelgiji baada ya kuondoka nchini mwake, ameshtakiwa kushiriki katika mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu na njama ya kuandaa uhalifu huo.
Iwapo atapatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Kesi ya Rwamucyo ni ya nane nchini Ufaransa kuhusiana na mauaji ya kimbari mwaka 1994, wakati inakadiriwa watu 800,000 - wengi wao wakiwa kabila la Watutsi waliuawa.
Rwamucyo, ambaye alikulia katika familia ya Wahutu, alifuatwa na wapiganaji wanaopinga Watutsi mwishoni mwa miaka ya 1980 baada ya kurejea kutoka masomoni nchini Urusi, kulingana na waendesha mashtaka, wanaomtuhumu kwa kueneza propaganda dhidi ya Watutsi.
Alipokuwa akifundisha chuo kikuu, pia alishiriki katika mauaji ya wagonjwa waliojeruhiwa na kusaidia kuwazika katika makaburi ya halaiki "katika jitihada za mwisho za kuharibu ushahidi wa mauaji ya kimbari", mwendesha mashtaka alisema, akinukuu taarifa za mashahidi.
Wakili wake, Philippe Meilhac, alisema Rwamucyo anakanusha kufanya makosa yoyote na anadai kuwa mashtaka hayo yanatokana na upinzani wake kwa serikali ya sasa ya Rwanda.
Ushiriki wake katika kuzika miili katika makaburi ya halaiki ulichochewa na nia ya kuepuka "shida ya kiafya" ambayo ingetokea ikiwa wangeachwa hadharani, wakili huyo alisema.