Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania Chadema. Picha/TRT Afrika. 

Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Chama cha upinzaniTanzania –CHADEMA kimeazimia kuanza maandamano iliyotaja kama ni ya amani kote nchini Tanzani kushinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa uchaguzi walioyatoa hivi karibuni. Maandamano hayo yamepangwa kuanza baadaye 24 mwezi huu.

Miswada inayopingwa na CHADEMA na ambayo imewasilishwa bungeni ni pamoja na ule wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 pamoja na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.5) Bill, 2023].

Muswada mwingine pia ni ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 [The Political Affairs Laws (Amendment) Bill, 2023].

Akitangaza msimamo huo, Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe alisema alikuwa muumini wa maridhiano ya amani kwa kuamini ndio mustakabli wa amani katika nchi, lakini sasa amejiridhisha kwamba maoni ya wananchi, viongozi wa dini, na mahakama imekiukwa baada ya kuwasilishwa kwa miswaada kadhaa Bungeni.

Mwenyekiti huyo wa chadema alifanya mkutano na waandishi wa habari katika ofisi mpya za chama hicho Mikocheni jijini Dara es Salaam, na maazimio hayo ni ya kikao cha Kamati Kuu kilichokutana kwa dharura kwa njia ya mtandao Januari 8, mwaka huu.

Uamuzi huo unakuja siku kadhaa baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji wa Maoni ya wadau lililojumuisha vyama vya siasa 18 vilivyosajiliwa, taasisi za dini, wananchi na asasi za kiraia zaidi ya 400.

Gharama za maisha

Kuhusu kupanda kwa ghrama za maisha nchini CHADEMA imeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kwa kupunguza tozo na kodi kwenye bidhaa na huduma muhimu kwa wananchi. Aidha ni kuondoa matumizi ya anasa na yasio ya lazima Serikalini, ili kuokoa mapato makubwa ya kodi ya wananchi ambayo amedai yanapotea kwenye matumizi yasio ya lazima.

“Inawezekana viongozi wa Serikali yetu wale wanaofanya maamuzi kwa niaba yetu wanaishi kwa maisha ya anasa, watoto wanasoma shule nzuri, hawana shida ya umeme, umeme unapokatika wao wana jenereta zinazoendeshwa kwa mafuta ya kodi ya wananchi, wao hawapandi daladala,” alisema Mbowe.

Alisema CHADEMA inaitaka Serikali kuja na mkakati mzuri wa kupunguza gharama za maisha ili fedha hizo ziokolewe zikawe pengine ruzuku ama kufidia eneo la kodi ambalo wananchi wanatozwa kupitia huduma kwenye bidhaa. Alirejea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali jinsi inavyopuuzwa na kutochukuliwa hatua kwa waliobainika kuhusika na ubadhilifu.

“Kwanzia leo naagiza viongozi wa chama wa mikoa yote ya Dar es Salaam na Tanzania kuanza maandalizi, tunataka serikli ijue kwa wakati huu tunamaanisha,” amesema Mbowe.

Kuhusu maandamano hayo Mbowe alionya kwamba ni safari yenye maumivu lakini ni ya lazima. ”Huu ni mwaka wa uchaguzi mpo tayari turudi tena kwenye uchaguzi kama wa mwaka 2019? “alihoji.

Kando ya mkutano uliotamatika Bungeni wa kukusanya maoni hapo juzi Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Dkt. Joseph Kizito Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa wadau wamejadili maudhui na kero zinazohusu maudhui hayo lakini alisisitiza maoni yatakayochukuliwa ni ambayo hayavunji katiba ya nchi.

“Maoni ambayo yatachukuliwa ni yale ambayo hayavuni katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pili yanaboresha miswada iliyopo,“ alisema kiongozi huyo wa kamati.

Maamuzi haya sio mageni lakini huenda yamekuwa na Sura tofauti. Mathalani, Katibu Mkuu wa chama hicho alionesha wazi kuwa hawakubaliani na baadhi ya mambo na kutoa pendekezo la kuondolewa kwa baadhi ya vipengele hasa, vinavyohusu uchaguzi pamoja na kile kinachotoa nafasi kwa wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi kwa kile alichokisema ni ‘kutokuwa na tija kwa vyama vya upinzani.'

John Mnyika, ambaye ni mbunge wa zamani wa majimbo ya Kibamba na Ubungo, alisema upinzani haukubaliani na muundo wa Tume uliopendekezwa kwenye sheria ambayo inaundwa na Rais, ambaye pia ni sehemu ya wagombea. Badala yake, Chama hicho kimependekeza sheria iweke wazi kuwa Tume iwe na wajumbe wenye uwakilishi bungeni.

Rais Samia Suluhu Hassa wa Tanzania, katika kuendeleza demokrasia nchini humo, amekuwa akisisitiza juu ya maridhiano na itakumbukwa mkutano wake wa mwaka jana na baadhi ya viongozi wa siasa jijini Dar es Salaam, aliruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara na ahadi ya kufanywa kwa marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya kisiasa na kuahidi kuukwamua mchakato wa katiba mpya.

TRT Afrika