Edward Lowassa aliwahi kufanya kazi chini ya Utawala wa benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete / Picha - X Edward Lowassa 

Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa amefariki.

Tangazo hilo limetolewa Jumamosi na Makamu wa Rais , Dkt. Philip Mpango kupitia televisheni ya taifa TBC.

''Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa amefariki Dunia leo February 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam,'' alisema Mpango.

Edward Lowassa, amabye amefariki akiwa na miaka 70, alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2008, akiwa chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Kuzaliwa na mwanzo wa masomo - Lowassa

Edward Ngoyai Lowassa, alizaliwa Agust 26 1953 - kijiji Ngarash, Wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha. Alikuwa mtoto wa nne kwa baba yake na amejaaliwa watoto watano na mke wake Regina Lowassa.

Lowassa alipata shahada yake ya kwanza ya sanaa katika elimu (Fine and Performing Arts) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977. / Picha : X - Edward Lowassa 

Alisomea shule ya msingi ya Monduli kati ya mwaka wa 1961 hadi 1967. Kisha akaendelea na masomo yake katika Shule ya Sekondari Arusha mwaka 1968 na kuhitimu Cheti chake cha O-Level, CSEE mwaka 1971. Kwa ngazi ya A Level, alisoma Shule ya Sekondari Milambo kuanzia mwaka 1972 hadi 1973 ambako alifuzu ACSEE.

Lowassa alipata shahada yake ya kwanza ya sanaa katika elimu (Fine and Performing Arts) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977.

Lowassa kisha akaenda kupata shahada ya Uzamili ya Masomo ya Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Bath nchini Uingereza mnamo 1984.

Akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikutana na Jakaya Kikwete na John Magufuli.

Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa aliwahi kufanya kazi ndani ya chama tawala CCM kama afisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya 1977 hadi 1989.

Nimekuwa na nitaendelea kuwa mstari wa mbele katika kusisitiza umuhimu wa Elimu bora na kwa wote, Elimu inayowaandaa vijana kuingia soko la ajira la dunia na pia kuwawezesha kujitegemea baada ya masomo.

Edward Lowassa

Baadaye aliajiriwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa kituo cha mikutano ya kimataifa Arusha AICC kuanzia 1989 hadi 1990

Maisha ya siasa

Lowassa alichaguliwa kuwa mbunge kupitia kundi la vijana ndani ya chama tawala CCM kati ya mwaka 1990 hadi 1995. Mnamo 1993 aliteuliwa kuwa waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu, na makamu wa kwanza wa Rais, haki na masuala ya Bunge.

Edward Lowassa Aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu wa Tanzania / Picha : X- Edward Lowassa 

Alihamishiwa Wizara ya Ardhi na makazi akiwa waziri mwaka 1993 hadi 1995.

Katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995, Lowassa alishinda ubunge kwa zaidi ya 87%, lakini hakupewa uteuzi serikalini kwa muda wa miaka miwili.

1997 -2000, Aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa alimteua Lowassa kuwa waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na kuondoa Umasikini, wizara ambayo imekuja kuvunjwa baadaye na kuundwa Wizara ya Mazingira.

Uchaguzi wa 2000, Lowassa aliwania kiti cha ubunge cha Monduli na kushinda. Baadaye Rais Mkapa akamteua kama waziri wa maji na mifugo, aliyoshikilia hadi mwaka 2005.

Kwenye uchaguzi wa 2005, aligombea tena ubunge na kushinda kwa kura 95%. Wakati huo chini ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete alimteua Lowassa kama Waziri mkuu wa Tanzania na akathibitishwa na wingi wa kura bungeni.

Hata hivyo Lowassa alilazimika kujiuzulu wadhifa wake 2008, kutokana na kuibuka kashfa ya Richmond, kampuni iliyothibitika kuwa ya watu binafsi huku serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha kupitia mikataba yenye mapungufu makubwa.

Edward Lowassa Aliawahi kuhudumu katika jeshi la taifa (TPDF) / Picha X- Edward Lowassa 

Lowassa alisema alichagua kujiuzulu kuhifadhi taswira ya serikali na chama chake, sio kuhusika binafsi katika ufisadi.

Kiu ya Urais

Lowassa aliwahi kuwania Urais mionogni mwa wana-CCM 17 waliotafuta tikiti hiyo mwaka 1995, japo wakati huo aliyeidhinishwa alikuwa Benjamin Mkapa.

Mwaka 2015, baada ya kushindwa juhudi kadhaa za kupata tikiti ya CCM, Lowassa alikihama chama cha CCM na kuingia katika upinzani CHADEMA.

Hata hivyo alikosa Urais huo kwa kushindwa na mpinzani wake kutoka CCM John Magufuli.

Hatimaye Lowassa alikitosa chama cha Upinzani CHADEMA na kurudi CCM.

Kumbu kumbu za Lowassa

  • Aliawahi kuhudumu katika jeshi la taifa (TPDF)

  • Alishiriki vita vya Uganda na Tanzania vilivyojulikana nchini Tanzania kama Vita vya Kagera na Uganda kama Vita vya Ukombozi vya 1979 kati ya Oktoba 1978 hadi Juni 1979 na kupelekea kupinduliwa kwa Rais wa Uganda Idi Amin.

  • Alikabidhiwa medali ya Nishani ya Vita.

  • Aliwahi kucheza katika bendi ya shule akiwa shule ya msingi.

TRT Afrika