Kiongozi wa Baraza linalotawala nchini Sudan Abdel Fattah al-Burhan amesema Alhamisi kuwa hakutakuwa na majadiliano wala maafikiano na makundi yanayokabiliana na serikali.
“Serikali haitowaacha wale walioamua kutuunga mkono na kupigana kwa lengo la kulinda heshima ,” Burhan alisema wakati wa ziara yake katika ngome ya jeshi iliyoko Omdurman. Magharibi mwa mji mkuu wa Khartoum.
“Watakuwa washirika kwa mipango yoyote ya kisiasa ya taifa hili. Hatutamtenga yeyote ,” aliongeza katika taarifa yake kama ilivyotolewa na jeshi.
"Hakutakuwa na majadiliano wala maafikiano na wale ambao wanapigana dhidi ya serikali na watu wake, na tunaendelea na safari yetu ya ushindi hadi pale tutakapokomboa kila sehemu ya nchi kutoka kwa vikosi vya RSF,” Burhan, ambaye pia ni mkuu wa jeshi, alisema.
Katika wiki za hivi karibuni Jeshi la Sudan limepata mafanikio makubwa dhidi ya RSF kwa kudhibiti mji wa Khartoum na majimbo mengine.
Kwa mujibu wa walioshuhudia, milipuko ilisikika katikati mwa mji wa Khartoum huku moshi ukionekana wakati wa mapambano kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa RSF.
Jeshi pia limepiga hatua kuelekea eneo la Soba, kusini mwa Khartoum, na kudhibiti daraja la Soba, ambalo linaunganisha Nile Mashariki na mji wa Khartoum, walioshuhudia walisema.
Jeshi na vikosi vya RSF wamekuwa wakipigana tangu katikati mwa mwezi Aprili 2023, vita vilivyosababisha mauaji ya watu zaidi 20,000 na wengine milioni 14 kuondolewa katika makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za maeneo hayo.
Hata hivyo utafiti kutoka vyuo vikuu vya Marekani, unakadiria kuwa watu takriban 130,000 wameuawa.
Jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zimetoa wito wa kumalizika kwa mapigano, wakionya kuwa hali inazidi kuwa mbaya huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na baa la njaa na wengine kufariki kutokana na uhaba wa chakula.
Mapigano hayo pia yanaendelea katika majimbo mengine 13 kati ya 18 ya Sudan.