Bunge la Ethiopia Jumanne lilipitisha mswada kuruhusu Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF), kujiandikisha upya na Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Ethiopia (NEBE).
Kundi hilo hapo awali lilipigwa marufuku kushiriki katika michakato ya kisiasa, baada ya kuanzisha vita dhidi ya serikali ya Ethiopia.
Sheria hiyo iliyorekebishwa, imepewa jina rasmi la “Usajili wa Uchaguzi, Vyama vya Siasa na Maadili ya Uchaguzi,” imepitishwa na wajumbe 547, huku wajumbe wawili wakipiga kura dhidi yake na mmoja kujiondoa.
Marekebisho hayo yanajumuisha vipengee vinavyoruhusu vyama vya kisiasa vinavyoshutumiwa kwa "kuendesha shughuli zao kinyume na sheria" kujiandikisha chini ya "masharti maalumu."
Wakati wa kikao cha bunge, mwakilishi wa serikali Tesfaye Belejge alisisitiza kuwa marekebisho hayo "yatawezesha vikundi ambavyo hapo awali vilitafuta mamlaka kutumia nguvu na silaha, kutafuta njia mbadala ya kisheria na ya amani."
Belejge pia alisisitiza kwamba mageuzi haya ni hatua muhimu kuelekea kudumisha amani nchini.
Siku ya Ijumaa, Getachew Reda, rais wa muda wa jimbo la Tigray, alipongeza serikali ya shirikisho ya Ethiopia baada ya Baraza la Mawaziri la nchi hiyo kuidhinisha mswada huo uliorekebishwa na kuutuma kwa watunga sheria kwa ajili ya kuidhinishwa.
"Azimio la Baraza la Mawaziri ni hatua sahihi katika kuimarisha amani," alisema kwenye X.
Mfumo mpya wa kisheria unabainisha mahitaji ambayo vyama vya kisiasa vinapaswa kutimiza ili kupata kutambuliwa kisheria, pamoja na jukumu la Tume ya Uchaguzi katika mchakato huo.
Bunge limelitambua kundi la TPLF kama kundi gaidi waliposhiriki vita vya kaskazini mwaka 2021, tume ya uchaguzi NEBE ilibatilisha usajili wake.
Hata hivyo, baada ya makubaliano ya Pretoria na kumalizika kwa mzozo huo mwishoni mwa 2022, wabunge walisitisha kulihusisha kundi hilo na ugaidi.
Mapema mwaka wa 2023, kiongozi wa zamani wa NEBE Birtukan Mideksa alikataa ombi la TPLF la kujiandikisha kama chama cha siasa, akidai kukosekana kwa vifungu vya kisheria vya kukipatia tena leseni chama kilichopigwa marufuku.