Mshindi wa tuzo ya Grammy mwigizaji wa dancehall kutoka Jamaica, Buju Banton amefichua kuwa asili yake ni ya Kinigeria.
Banton, ambaye jina lake halisi ni Mark Myrie, alisema hayo alipokuwa mgeni kwenye podcast Drink Champs, iliyoandaliwa na N.O.R.E. na DJ EFN.
Alisema damu yake ilifuatiliwa, na alikuwa ni "Mtu wa kutoka Igbo" asili yake inatoka kusini-mashariki mwa Nigeria.
“Kizazi changu kilitoka Nigeria. Mimi ni jamaa wa Igbo kulingana na damu yangu,” alisema kwenye podikasti hiyo.
Lakini labda jambo kuu alilolizungumzia katika podcast ni maoni yake juu ya ushawishi unaokua wa Afrobeats.
Katika mahojiano hayo, Buju Banton anasema Afrobeats wanapaswa kufanya zaidi kwa kupongeza vuguvugu la reggae na dancehall kwa ushawishi wao chanya, ambao umewapa Afrobeats faida ya kimataifa.
Asili kamili ya Afrobeats na vishawishi vyake vya muziki bado ni mjadala mkali, kwani mitindo tofauti ya muziki ya kimataifa inadai kuwa na jukumu katika utoaji wa muziki wa kipekee wa Afrobeats na mvuto wa kimataifa.
Banton alisema wasanii wa muziki wa Afrobeats wanapaswa kuinua ushawishi wao wa kimataifa na kuzungumza kwa nguvu zaidi kuhusu masuala ya kijamii ambayo huathiri Waafrika.
"Wasanii barani Afrika wanahitaji kuleta athari na muziki wao. Hakuna wimbo hata mmoja katika Afrobeats, ambao ninaweza kusema ni wa kutoka Afrika. Wasanii ninaowaheshimu barani Afrika ni Fela Kuti, Youssou N’Dour, Lucky Dube kutoka Afrika Kusini, Salif Keita na Baaba Maal.
Alilaumu Afrobeats kwa kuwavunja moyo Wajamaika katika juhudi zao za kuungana na dunia nzima licha ya watu kufurahia na kupenda dancehall na reggae.
Mnamo 2011, Banton alishinda Grammy ya Albamu Bora ya Reggae kwenye Tuzo za 53 za Grammy huko Los Angeles.