Tinubu

Bola Tinubu aliapishwa kama rais wa Nigeria siku ya Jumatatu katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu Abuja. Anakuwa kiongozi wa 16 wa taifa hilo tangu uhuru.

Mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 71 alishinda uchaguzi wa urais mwezi Machi kwa asilimia 37 ya kura, kulingana na matokeo rasmi.

Anachukua nchi ambayo inapambana na mfumuko wa bei unaoongezeka na ukosefu wa ajira kwa vijana, pamoja na changamoto za usalama ambazo zimeonekana kuongezeka katika visa vya utekaji nyara kwa ajili ya fidia.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa pamoja na marais wa Algeria, Ghana, Chad, Niger, Burundi, Rwanda, Tanzania na Sierra Leone walikuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika walioshuhudia tukio hilo.

Katika kiapo chake, Tinubu aliahidi kuheshimu katiba na kutekeleza mamlaka yake ya urais kwa ukamilifu.

Katika hotuba yake ya kuapishwa, rais alisema atafutilia mbali ruzuku ya muda mrefu kwa bidhaa za petroli, kupunguza kiwango cha riba, kuwianisha ushuru, kuunda ajira mpya milioni moja, kujenga vituo vya kilimo na kufanya gharama ya umeme kuwa nafuu zaidi.

Wakati huo huo, Tinubu alisema ataboresha viwango vya ubadilishaji wa sarafu na kuja na sera zinazopendelea viwanda vya ndani ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

"Sitaruhusu masilahi yangu ya kibinafsi kuathiri mwenendo wangu rasmi au maamuzi yangu rasmi," alisema wakati wa kula kiapo.

Matamshi yake yanakuja kutokana na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini Nigeria, huku kampuni ya ukaguzi ya KPMG ikisema kwamba kiashiria cha ukosefu wa ajira nchini humo mwaka 2022 kilisimama kwa asilimia 37.7, ambacho kinaweza kuongezeka hadi asilimia 40.6 ifikapo mwisho wa 2023.

Makamu wa Rais Mpya wa Nigeria Kashim Shettima pia alikula kiapo siku ya Jumatatu ili kumsaidia Tinubu kutimiza manifesto yake.

Tinubu anachukua nafasi kutoka kwa Muhammadu Buhari ambaye muhula wake wa pili na wa mwisho ulimalizika Mei 29.

TRT Afrika