Makubaliano hayo yanajumuisha faini ya hadi dola milioni 243 za Marekani kulipwa kama fidia kwa familia za waathiriwa./ Picha : Reuters 

Kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing imeingia makubaliano na mahakama kukubali lawama kwa shtaka la uzembe uliosababisha ajali za ndege na kuuwa watu 346 kati ya 2018 na 2019.

Makubaliano hayo yanasema kuwa Boeing imekubali shtaka la udanganyifu wa jinai kwa ndege zake aina ya 737 max jet zilizoanguka nchini Indonesia na Ethiopia.

Makubaliano hayo yanajumuisha faini ya hadi dola milioni 243 za Marekani kulipwa kama fidia kwa familia za waathiriwa.

Mahakama iliamua kuwa Boeing ilivunja makubaliano ya awali ambapo kampuni hiyo iliweza kukwepa kufunguliwa mashtaka ya uhalifu.

Kampuni hiyo ilishutumiwa kwa kukiuka oparesheni za usalama za ndege zake ambazo zilisababisha moja kwa moja ajali za ndege nchini Indonesia na Ethiopia.

Hata hivyo chama cha familia za waathiriwa kimekashifu makubaliano hayo kikisema ina maana kuwa kampuni hiyo imekwepa kujibu mashtaka mahakamani. Pia emelalamika kuwa hakuna maafisa wahusika binafsi walioshtakiwa badala ya kampuni peke yake.

Ndege ya Ethiopian Airlines nambari 302 ilikuwa imeratibiwa kwa safari ya kimataifa ya abiria kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya.

Mnamo tarehe 10 Machi 2019, ndege ya Boeing 737 MAX 8 iliyokuwa ikiendesha safari hiyo ilianguka karibu na mji wa Bishoftu dakika sita baada ya kupaa. Abiria wote 149 na wahudumu 8 waliokuwemo ndani walikufa.

Flight 302 ndiyo ajali mbaya zaidi ya Ethiopian Airlines kufikia sasa

Boeing ilikuwa imefanya makubaliano na Mahakama kulipa fidia kwa familia na kuimarisha usalama wake, na badala yake isifunguliwe mashtaka ya uhalifu.

Mashaka yasiyoisha

Hata hivyo maafisa wamesema mwanzoni mwa mwaka huu kuwa Boeing haikutimiza makubaliano hayo.

Si hayo tu, ilijikuta tena matatanoi baada ya ndege nyingine aina hiyo ya 737 MAX kupoteza mlango wake ikiwa angani. Uchgunguzi wa tukio hilo bado unaendelea pembeni.

Umuhimu wa makubaliano hayo

Iwapo yataidhinishwa na jaji wa mahakama ya kitaifa wa marekani, ina maana Boeing itaorodheshwa kama kampuni ya kihalifu.

Italipa faini ya dola milioni 243 na kushurutishwa kuwekeza mamilioni zaidi katika kuimarisha oparesheni zake za kiusalama na usalama wa ndege zake.

Itashurutishwa kumteua mkaguzi huru kwa muda wa miaka mitatu atakayetoa ripoti kwa seirkali kila mwaka juu ya usalama wa ndege hizo.

Waliofariki katika ajali ya ndege ya Ethiopian Airline mwaka 2019 ni Wakenya 32, Wakanada 18, Waethiopia tisa na Wamarekani wanane.

TRT Afrika