Na Ronald Sonyo
TRT Afrika, Dodoma, Tanzania
Benki Kuu nchini Tanzania imesema inakusudia kuanza kupokea sarafu zenye thamani ya kuanzia shilingi 50, 100 na 200 katika muda wa mwezi mmoja.
Benki hiyo imesema, lengo la kufanya hivyo, ni kufuatia utafiti uliofanywa ambao ulibaini kuwa, sarafu hizo mara nyingi hazitumiki katika mzunguko wa fedha nchini humo.
"BENKI kuu ya Tanzania (BoT) imefanya utafiti na kugundua uwepo wa sarafu nyingi ambazo hazitumiki kwa muda mrefu katika mzunguko wa kiuchumi na badala yake zimeendelea kusalia nyumbani, ofisini, kweye magari, biashara na taasisi mbalimbali nchini Tanzania," imesema taarifa ya BoT.
Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanasema tangazo hilo linamaanisha fedha ya Tanzania imeendelea kushuka thamani na kwa sasa haziwezi tena kutumika katika mzunguko wa manunuzi.
“Kiuhalisia Benki Kuu imeamua kuziondoa sokoni kwa sababu fedha hizo hazitumiki. Kwa sasa ukimlipa mtu shilingi 50, au 100 upokeaji wake unakuwa sio mzuri. Thamani ya hizo sarafu imeondoka na thamani ya fedha ikiondoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huitoa katika mzunguko,” amesema Dk Nassibu Mramba, mhadhiri katika Chuo cha Elimu ya Biashara.
Hata hivyo BoT iliutetea uamuzi wake kuwa ni katika jitihada za kuendelea kutunza sarafu dhidi ya uharibifu unaotokea katika mazingira yasiokuwa salama na kuirudisha katika mzunguko wa fedha.
“Huduma hii itatolewa kama zoezi maalumu la mwezi mmoja” Ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia ambayo imetolewa katika tovuti ya Benki na ambayo TRT ilipata nakala yake haikufafanua zaidi, ila imewataka wananchi kuitilia maanani.
Mara ya mwisho, Benki ya Tanzania kufanya mabadiliko ilikuwa ni mwaka 2014, ambapo iliondoa noti za shilingi 500 na badala yake kuweka sarafu ya 500 kwa madai kwamba, noti hizo zinapitia sehemu nyingi hivyo uharibifu wake ni wa haraka ikilinganishwa na sarafu.
Ingawa sarafu ya shilingi 50, 100, na 200 zinapatikana katika mzunguko wa fedha, lakini ni miaka mingi tangu kutolewa. Sarafu ya shilingi 200 iliingizwa sokoni mwaka 1998. Wakati huo, ilikuwa ndio sarafu (coin) yenye thamani kubwa nchini Tanzania.
Noti halali zinazotumika nchini Tanzania ni kuanzia ya shilingi 500, 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000 ambayo ndio ya juu zaidi.