Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa./Picha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema kuwa litatoa maamuzi juu ya Palestina kuwa mwananchama kamili wa umoja huo, mwezi huu.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ya 'kihistoria', huku machafuko katika eneo la Gaza yakifikisha miezi saba.

Balozi wa Malta ndani ya Umoja wa Mataifa Vanessa Frazier, alisema kuwa "baraza hilo limeazimia kutoa maamuzi hayo ndani ya mwezi wa Aprili."

Ombi lolote la kujiunga na Umoja wa Mataifa ni lazima lipitie ndani ya Baraza la Usalama, ambamo Marekani, ambaye ni mshirika mkubwa wa Israel ana kura ya turufu, kabla ya kupitishwa na mkutano mkuu.

Wapalestina, ambao wamekuwa na hadhi ya waangalizi katika baraza hilo la dunia tangu mwaka 2012, wameshawishi kwa miaka kadhaa kupata uanachama kamili, jambo ambalo lingekuwa sawa na kutambuliwa kwa taifa la Palestina. Takriban asilimia 72 ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa tayari wanaitambua Palestina kama nchi.

"Huu ni wakati wa kihistoria," mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Palestina Riyad Mansour aliwaambia waandishi wa habari wakati wajumbe wa Baraza la Usalama, kupitia kamati ya muda kuhusu wanachama wapya, walianza mchakato wa mapitio baada ya Wapalestina wiki iliyopita kuzindua upya zabuni yao rasmi ya 2011.

Marekani na kura ya turufu?

"Tunachoomba ni kuwa na nafasi yetu halali miongoni mwa jumuiya ya mataifa, kutendewa sawa - sawa na mataifa mengine, kuishi kwa uhuru na heshima, kwa amani na usalama, katika ardhi ya mababu zetu," alisema Mansour wakati wa Mkutano Mkuu.

"Tunatumai kuwa baada ya miaka 12 tangu tubadili hadhi yetu ya kiuangalizi, Baraza la Usalama litajiinua kutekeleza makubaliano ya kimataifa juu ya suluhisho la serikali mbili kwa kulikubali taifa la Palestina kwa uanachama kamili," mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Palestina Riyad Mansour aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo.

Hata hivyo, waangalizi wanatabiri kura ya turufu kutoka kwa Marekani, ambayo imepinga uanachama wa Palestina tangu 2011.

"Msimamo wetu unajulikana, na haujabadilika," balozi wa Marekani ndnai ya Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema. "Lakini tutaendelea kutafuta njia ya kuwa na serikali mbili."

Hata hivyo mjumbe wa Malta Frazier alisema "mchakato wa kamati hiyo ulikuwa na thamani sana, na kuongeza kuwa kamati hiyo itakutana tena siku ya Alhamisi.

TRT Afrika