Baraza jipya la mawaziri la Afrika Kusini limeapishwa siku ya Jumatano, wakati ambapo serikali ya nchi hiyo inakabiliana na changamoto ya uchumi na mabadiliko ya kijamii.
Mwanasheria Mkuu Zondo alisimamia zoezi hilo la kuwaapisha wajumbe mawaziri 32, mjini Cape Town.
Rais Cyril Ramaphosa alizindua baraza hilo la mawaziri katika serikali ya Umoja wa Kitaifa siku ya Jumapilu, na kumteua tena Paul Mashatile kama makamu wake.
Hata hivyo, kiongozi huyo amekosolewa kwa ukubwa wa baraza, linalohusisha manaibu mawaziri 43.
Kwa jumla, vyama saba vilipokea nyadhifa za mawaziri katika baraza la mawaziri. Mawaziri 20 walitoka chama cha African National Congress (ANC), sita kutoka Democratic Alliance (DA), wawili kutoka Inkatha Freedom Party na mmoja kila mmoja kutoka vyama vya GOOD, Freedom Front Plus, Patriotic Alliance na Pan Africanist Congress ya Azania.
Zoezi hilo linakuja mwezi mmoja baada ya ANC kupoteza wingi wake wa wabunge katika uchaguzi wa Mei, na kulazimisha kuunda serikali ya mseto.