Umoja wa Afrika umetoa ripoti yake ya kwanza baada ya waangalizi wake kutembelea vituo tofauti vya uchaguzi mkuu nchini Afrika Kusini wakati wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
"Wananchi wa Afrika Kusini walitumia kwa uhuru haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na walipiga kura kwa amani," amesema rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ndiye aliyeongoza timu ya waangalizi wa Umoja wa Afrika.
Chama tawala cha African National Congress, ANC kinaongoza kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizohesabiwa. Hata hivyo, matokeo ya awali yanaonyesha, chama hicho kikongwe kimepoteza uungwaji mkono. Chama cha Democratic Alliance kinashika nafasi ya pili huku chama cha Umkhonto weSizwe (MK) cha Rais wa zamani Zuma kwa sasa kinashika nafasi ya tatu.
"Kushiriki kwa vijana na wanawake kunatoa matumaini kwa mustakabali wa demokrasia barani Afrika na kunaonyesha imani iliyoongezeka katika mchakato wa uchaguzi. Wakati mchakato wa uchaguzi bado unaendelea," ameongezea.
Kati ya watu milioni 62, watu milioni 27.79 walijiandikisha kupiga kura. Kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini, IEC, waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 58.58 ikiwa na maana kwamba, waliojitokeza kupiga kura ni takriban milioni 16.2.
Timu 21 za waangalizi 65 zilitumwa na AU katika majimbo tisa kufuatilia upigaji kura maalumu tarehe 28 Mei na upigaji kura tarehe 29 Mei 2024, ukiangazia vipengele mbalimbali vya mchakato wa uchaguzi.
Upigaji kura maalumu ulifanyika ili kuwapa nafasi wapiga kura ambao hawakuweza kutembelea vituo vya kupigia kura siku ya kupiga kura.
Hawa ni pamoja na wale wanaofanya kazi siku maalumu ya kupiga kura, wagonjwa, wazee, walemavu, au mama waja wazito.
Maoni ya AU kwa uchaguzi
Ujumbe huo umetaka masuala ambayo hayakuonekana kuwa sawa wakati wa uchaguzi.
Ujumbe ulibaini kuwa kulikuwa na hatua mbadala ya kutumia orodha ya mwongozo kwa ajili ya kuthibitishwa kwa wapiga kura.
Masanduku ya kura yalikuwa madogo na hayakutosha.
Katika baadhi vituo masanduku yanasemekana, yalikuwa na maandishi hafifu au hayakuwekwa alama. Hili lilifanya yasitambulike, na kuchangia kuongeza muda wa kupanga na kuhesabu.
Waangalizi wa AU walibaini kulikuwa na mahema ya kampeni ya vyama vya siasa nje ya vituo vya kupigia kura, jambo ambalo linaweza kuwatia hofu wapiga kura au kushawishi maamuzi yao.
Zaidi ya hayo, waangalizi wa AU wanasema foleni ndefu, hasa katika vitongoji vyenye msongamano mkubwa na vitongoji vya mijini, vilichangia kufadhaika miongoni mwa wapiga kura.
Vituo vingi vya kupigia kura viliwahudumia wapiga kura baada ya muda rasmi na kuingia katika saa za mapema za siku iliyofuata.
"Tunawasihi wahusika wote watakaokuwa na malalmiko yoyote kutumia mbinu zilizopo za kutatua mizozo ya uchaguzi kushughulikia malalamishi yao," Kenyatta ameongezea katika taaria hiyo.
Ripoti ya mwisho wa Umoja wa Afrika yenye maelezo ya kina na mapendekezo itatolewa miezi miwili baada ya uchaguzi.