Mkutano wa Umoja wa Afrika kuhusu Amani na Usalama, 2024. Picha na AU PSC. 

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Umoja wa Afrika unaunda mfumo wa kusaidia nchi ambazo zimesimamishwa kwa muda katika Umoja wa Afrika ili ziwe katika kipindi cha mpito wakati zikijiandaa kufikia utawala wa kidemokrasia.

Baraza la Amani na Usalama la AU, lenye wajumbe 15, lilifanya mkutano wake katika mkutano wa kila mwaka wa marais, nchini Ethiopia tarehe 17 na 18 Februari 2024.

"Tutafanya kazi na wahusika wengi ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP, katika uzinduzi wa kile tunachokiita "Mfumo wa Afrika," hii ni kusaidia mabadiliko ya amani barani Afrika," anasema Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Bankole Adeoye.

Hadi sasa nchi sita za Afrika zilizo uanachama wao umesimamishwa kwa muda Umoja wa Afrika ni Gabon, Niger, Guinea, Sudan, Burkina Faso, na Mali. Wote wako chini ya utawala wa kijeshi.

Sheria ya AU inaunga mkono utawala wa kiraia katika nchi wanachama wake.

"Hatua hii inakuza ushirikiano wa jinsi nchi wanachama waliosimamishwa kwa muda kutoka AU, wanaweza kuwa na mpito wa kisiasa bila changamoto. Kwa hivyo, tunafanya kazi na nchi husika katika suala la ajenda yao ya mpito wa kisiasa ili waweze kurejea AU. Hii ni kwa masharti kwamba waheshimu utaratibu wa kikatiba na kufanya uchaguzi huru, haki na uwazi,” Adeoye anaongeza.

Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS, iliiwekea vikwazo nchi za Mali, Burkina Faso na Guinea baada ya mapinduzi ya serikali / Picha kutoka ECOWAS 

Vikwazo hutolewa kufuatia sheria zinazosimamia muungano wa bara. Walakini, wataalam wanatilia shaka ufanisi wao.

"Lakini nyakati zimebadilika, na viongozi wa kijeshi wana sababu kidogo sana ya kuogopa kutokuwa katika Umoja wa Afrika," hayo ni kwa mujibu wa uchambuzi wa Crisis Group. International Crisis Group ni Shirika Huru linalofanya kazi kuzuia vita na kuunda sera ambazo zitajenga dunia yenye amani zaidi.

"… Ulimwengu wa ushindani mkubwa wa kijiografia unafanya iwe rahisi kwao kuhusiana na nchi tofauti za kigeni kwa manufaa yao ya kisiasa," imeongeza.

Nchi za Afrika Magharibi - Mali, Niger na Burkina Faso zimefanya uamuzi wao wa kujiondoa mara moja kutoka kwa Umoja wa Afrika Magharibi, ECOWAS, ambacho ni chombo cha utekelezaji cha AU.

Wamelalamikia masuala tofauti ikiwemo kile wanachokiita kutotendewa haki na ECOWAS.

Lakini Umoja wa Afrika unaonekana bado una nia ya kuweka vikwazo kama kipaumbele katika kushughulikia mabadiliko ya serikali kinyume na katiba.

"AU haifanyi chochote kipya," anasisitiza Adeoye," ni muhimu kutambua kwamba, ndiyo, wahusika wa mapinduzi ya kijeshi wanaweza kutoa sababu mbalimbali kwa sisi katika AU kukiuka maadili katika mifumo ya kawaida, lakini vikwazo vitaendelea kuwekwa kwa masharti ya kusimamishwa kutoka AU."

Jopo la ngazi ya juu kwa Sudan

Mzozo wa Sudan ulifanikisha suala lililojadiliwa na Baraza la Amani na Usalama la AU katika ngazi ya urais huku ikitajwa kama "kipaumbele kikuu cha AU mnamo 2024".

Vita kati ya majeshi ya Sudan na Vikosi vya Rapid support Forces tangu Aprili 2023 yameitumbukiza nchi hiyo katika hali mbaya ya kibinadamu / Picha: Reuters

Mapigano kati ya majeshi ya Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka tangu Aprili 2023 yameitumbukiza nchi hiyo katika kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa "mgogoro wa dharura."

"Miezi kumi tangu mzozo huo kuibuka, nusu ya wakazi wa Sudan - baadhi ya watu milioni 25 - wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Zaidi ya watu milioni 1.5 wamekimbia mipaka ya Sudan hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini," hayo ni kulingana na Shirila la Umoja wa Mataifa la UNHCR.

Juhudi za upatanishi zimegonga mwamba huku nchi hiyo ya pembe ya Afrika, iliyosimamishwa uanachama wa Umoja wa Afrika, ikiamua Januari 2024, kusimamisha uanachama wake kutoka kwa Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD.

IGAD ilipewa jukumu na Umoja wa Afrika kuongoza juhudi za upatanishi kati ya pande zinazozozana.

Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika 2024 umeidhinisha kikundi cha ngazi ya juu kwa Sudan.

Kikundi hicho kitajumuisha Dkt. Mohamed Ibn Chambas, Mwakilishi Mkuu wa AU anayehusika na mfumo wa AU wa " kunyamazisha Bunduki, pia ni pamoja na Dkt. Specioza Wandira-Kazibwe, Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Uganda na Balozi Fransisco Madeira, aliyekuwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Umoja huo nchini Somalia na aliyekuwa Mkuu wa ATMIS.

"Tuna watu katika kanda ambao wanaijua Sudan hivyo wanaweza kuchangia kupata suluhisho. Ninaweza kuwahakikishia kuwa jopo hilo sasa liko tayari kutekeleza shughuli zake kutoka kwa mkutano huu wa kilele ili kuhakikisha kuwa washikadau wote ... nchini Sudan wanachangia katika mazungumzo ya amani ya kisiasa,” Adeoye ameongezea.

Ni matumaini ya viongozi hao wa AU kuwa mazungumzo ya kisiasa nchini Sudan yatasaidia kuhamasisha kuwaleta wadau wote mezani na hatimaye kusitisha vita, nchini Sudan.

Umoja wa Afrika unatumai kuwa mwaka huu utasaidia kuunga mkono nchi ambazo ziko chini ya utawala wa kijeshi kuweka utaratibu wa wazi utakaosaidia kufanyika kwa uchaguzi ili mamlaka ziweze kuhamishiwa kwa ŕaia na waweze kuŕejeshwa tena kushiriki katika shughuli za Umoja wa Afŕika.

TRT Afrika