AU, IGAD, UN wanataka mpango mmoja kupata amani Sudan

AU, IGAD, UN wanataka mpango mmoja kupata amani Sudan

Umoja wa Afrika inataka kutimiza mpango wake wa kutatua mzozo nchini Sudan
Kikao cha Ufunguzi: Mkutano wa Tatu wa Utaratibu Uliopanuliwa wa Mgogoro wa Sudan: Picha: AU

Vita nchini Sudan vinaendelea tangu tarehe 15 Aprili mwaka huu kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Rapid Support Forces, RSF.

Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, IGAD, wamejadili jinsi ya kutekeleza mfumo wa utatuzi wa mzozo nchini Sudan.

Umoja wa Afrika unatambua utawala wa kiraia pekee na unasema Sudan lazima iungwe mkono ili kurejea katika mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia.

Hadi sasa Marekani na Saudi Arabia zimewezesha makubaliano kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Rapid Support Forces kwa ajili ya kusitisha mapigano.

Mnamo tarehe 20 Mei walikubaliana kusitisha mapigano kwa siku saba ambayo baadaye waliongeza mpaka tarehe 29 Mei kwa siku 5.

"Tunahitaji kutafakari jinsi tunavyobadilisha mchakato huo kwa msingi wa ushiriki mpana kwenda mbele zaidi na ushiriki ambao utakuwa wa pamoja ambao utafanya usitishaji kamili wa mapigano," anasema Dkt. Mohamed Sarjoh Bah, Mkurugenzi wa Kitengo cha uchunguzi wa mizozo katika kamisheni ya Umoja wa Afrika.

Mpango wa Umoja wa Afrika ya kutatua mzozo nchini Sudan uliundwa tarehe 27 Mei wakati baraza la amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilipokutana katika ngazi ya marais.

Katika mkutano huo ulioongozwa na rais wa Uganda Yoweri Museveni, Umoja wa Afrika ilisisitiza umuhimu wa kuwa na mchakato mmoja wa amani wa Sudan.

Wakuu wa nchi za Afrika walisema mchakato huo lazima uratibiwe chini ya mwamvuli wa pamoja wa Umoja wa Afrika, IGAD, ligi ya nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa.

"Kuongezeka kwa mipango ya upatanishi hakuta hudumia maslahi ya amani ya watu wa Sudan," Workeneh Gebeyu, katibu mtendaji wa IGAD amesema.

"Umoja wa Mataifa unapendekeza jopo kwa pamoja la watu watatu au wanne wa ngazi ya juu kusaidia kuongoza na kuratibu mchakato utakaoundwa wa amani Sudan. Utaratibu wa pande tatu za IGAD, AU na UN zinapaswa kufanya kazi chini yao na kuunga mkono juhudi zao,” alisema Gerald Mitchell, Naibu Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa mataifa UNOAU.

Umoja wa Mataifa umependekeza kuwa ofisi maalumu iundwe haraka iwezekanavyo ili iweze kuratibu moja kwa moja na kuunga mkono mipango yote ya kusaidia mchakato madhubuti wa amani na mazungumzo ya kisiasa nchini Sudan

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema atatuma wajumbe katika mataifa jirani ya Sudan ili kuimarisha utafutaji wa mbinu ya pamoja ya kutafuta suluhu endelevu la mgogoro wa tabaka mbalimbali nchini Sudan.