Ernest Bai Koroma aliyekuwa rais wa Sierra Leone. 

Aliyekuwa rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma, aliyeshtakiwa kwa kile kinachodaiwa na mamlaka kuwa alishiriki katika jaribio la kupindua serikali, ameondoka nchini humo na kufika Nigeria siku ya Ijumaa.

Koroma, aliyeongoza taifa hilo la Afrika Magharibi kuanzia 2007 hadi 2018, alipata ruhusa kutoka Mahakama Kuu kwenda kutibiwa nchini Nigeria kwa muda usiozidi miezi mitatu.

Rais wa sasa Julius Maada Bio katika hotuba yake kwa taifa Alhamisi usiku alisema hatua hiyo ya mahakama ilikuwa ishara ya ubinadamu.

Koroma amefika mjini Abuja Ijumaa jioni, akikaribishwa na Mshauri wa Ulinzi wa Taifa Nuhu Ribadu na rais wa ECOWAS Kamishna Omar Alieu Touray, kwa mujibu wa mwandishi wa AFP.

Mahakama Kuu nchini Sierra Leone ilitoa kibali kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo kupata matibabu nchini Nigeria kwa muda usiozidi miezi mitatu tangu tarehe ya kutolewa kwa kibali hicho, na anatakiwa kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu afya yake.

Koroma, ambae amekuwa katika kifungo cha nyumbani tangu Disemba 9, alishtakiwa mapema Januari kwa makosa manne ikiwemo uhaini unaohusiana na tukio la mwezi Novemba.

November 26, wanajeshi walishambulia ghala la silaha, kambi mbili, magereza mawili na vituo viwili vya polisi, na kukabiliana na vikosi vya ulinzi.

Watu 21 waliuawa na mamia ya wafungwa kutoroka kabla ya mamlaka kuweza kudhibiti upya baada ya kile walichosema ilikuwa ni jaribio la mapinduzi lililofanywa na sehemu ya vikosi vya jeshi.

Takriban watu 80 walikamatwa kufuatia tukio hilo, wengi wao wakiwa wanajeshi.

TRT Afrika