Watu wakiandamana katika sherehe, Berlin, Ujerumani, Agosti 29, 2018, kukabidhi mabaki ya binadamu kutoka Ujerumani kwa Namibia kufuatia mauaji ya halaiki ya mwaka 1904-1908 dhidi ya Herero na Nama. Picha/REUTERS/Christian Mang / Photo: Reuters

Na Yahya Habil

Na Yahya Habil Hivi karibuni, ofisi ya Rais nchini Namibia ilitoa taarifa ya kupinga na kulaani vikali kauli ya Ujerumani yenye kuunga mkono mauji ya kimbari na ubaguzi wa wazi wa taifa la Israeli dhidi ya raia wasio na hatia mjini Gaza.

Kauli hiyo ilikuja baada ya Ujerumani kupinga kesi dhidi ya Israeli, iliyofunguliwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Namibia iliikumbusha dunia, kupitia mtandao wa X mauaji ya watu wake yaliyofanywa na Ujerumani, kama tukio la kwanza la kimbari Namibia kutokea katika karne ya 20(1904-1908).

Nchi hiyo ilisisitiza kuwa iwapo Ujerumani haijawajibika kutokana na uovu ilioutenda dhidi yake, haina msingi wowote wa kuzungumza chochote, hasa linapokuja suala la mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kulingana na Rais wa Namibia, hii ni kwa sababu Ujerumani haiko tayari kujifunza kutokana na makosa yake ya awali.

Ukosoaji wa Namibia na uamuzi wa Afrika Kusini ni uthibitisho tosha kuwa bara la Afrika limeazimia kuwa vinara wa kulinda sheria za kimataifa na sauti yenye mamlaka dhidi ya uhalifu wa kibinadamu duniani.

Kimsingi, nchi za Afrika ndizo zilizosimama kidete na kuwa sehemu muhimu ya azimio namba 3379, la Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lililotangaza Uzayuni kama aina ya ubaguzi wa rangi.

Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni Gambia iliiburuza Myanmar katika mahakama ya ICJ kwa tuhuma za mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Rohingya.

Na matokeo yake, nchi za Kiafrika sasa zinafunika ombwe lililotanda duniani baada ya mataifa ya Magharibi kushindwa kutimiza majukumu yao kwa kupoteza dira na mielekeo yao.

Zaidi ya hayo, ni jambo la kawaida kushuhudia mataifa ya Afrika yakiongoza vita dhidi ya ukandamizaji na ukoloni kwani matukio ya mwisho ya kutisha zaidi yalitokea barani humu.

Kwa maneno mengine, Waafrika wanatambua vizuri sana adha ya ukoloni na ndiyo maana hawataki kurudi nyuma.

Na linapokuja suala la suala la udhalimu wa Israeli dhidi ya wapalestina mjini Gaza, haishangazi, kuona Afrika Kusini ikichukua jukumu hilo kubwa.

Kutoka kifungoni

Maamuzi ya Afrika Kusini yanakuja wakati muafaka wakati nchi hiyo bado ina majeraha na malalamiko ya ubaguzi wa rangi uliotawala nchi hiyo kati ya 1948 na 1991, ambayo kimsingi, ni sheria inayotawala ndani ya ardhi ya Israeli ambayo nayo ilianzishwa mwaka 1948.

Na hivi leo, Afrika Kusini imejivua minyororo ya ubaguzi wa rangi na inaongozwa na watu wale wale walioendesha mapambano dhidi ya aina hiyo ya udhalimu ambao ulikuwa sehemu ya Israeli.

Ingawa haikutajwa kwenye kauli ya Rais wa Namibia mwenyewe, ni vizuri kufahamu kuwa nchi hiyo pia ilipitia madhila kama ya majirani zao, Afrika Kusini. Ikumbukwe pia kuwa Namibia, hadi kufikia 1990, ilikuwa chini ya udhibiti na mamlaka ya serikali ya Afrika Kusini.

Kwa hiyo, Namibia pia ina msimamo huo huo kama wa Afrika Kusini kwani ilikumbwa na utawala wa ubaguzi wa rangi na , na mauaji ya halaiki yaliyofanywa dhidi ya watu wake mwanzoni mwa karne ya 20, ambayo yalishuhudia adhabu ya pamoja ya watu wa Herero na Namaqua.

Kama mtu anavyoweza kudhani, matukio ya mauaji haya ya kimbari yanafanana na yale yaliyotokea Gaza, na hivyo kuipa Namibia sababu nyingine ya kusimama dhidi ya vitendo vya Israeli.

Hofu ya Ujerumani

Namibia, kama tu ilivyo kwa Afrika Kusini inaionesha dunia kuwa fundisho ililopata kutoka kwenye makucha ya ukoloni haliendi bure na ndio maana inasimama kwa ajili ya Wapalestina na watu wote wanaopitia udhalimu na ukandamizwaji.

Nchi hiyo ina uwezo na sababu nzuri tu ya kupata mafunzo kutokana na historia yake yenyewe.

Namibia ilitambua ya kwamba uhuru wake ulitokana na mauaji ya kimbari kutoka kwa watawala wao, na kuwa si vyema kwa jambo kama hilo litokee popote pale duniani.

Na kwa upande mwingine, Ujerumani haikuwa tayari kukubali kwamba mauaji ya kimbari na udhalimu kwa jamii yoyote ile ya watu, sio kwa Wayahudi tu, haufai, bila kujali muktadha wake.

Badala yake, nchi hiyo inaendelea kufumbia macho yale yanayoendelea Palestina, ikihofia kuingizwa kwenye mkumbo huo huo.

Hili halishangazi kwani baada ya vita vya pili vya dunia sera ya mambo ya nje ya Ujerumani, vimeiweka nchi hiyo mbali na kujihusisha na uvamizi haramu na udhalimu.

Uhalifu wa ndani

Hata hivyo, kwa kuiunga mkono Israeli siku za karibuni, Ujerumani inarejesha taswira yake halisi ya mvamizi na mdhalimu, bila yenyewe kujua.

Kwa upande wa Namibia na bara la Afrika kwa ujumla, safari bado ni ndefu ya kubakia sauti ya mamlaka dhidi ya udhalimu duniani, licha ya juhudi zinazofanyika.

TRT Afrika