Rwanda imeweza kufanya maendeleo huku ikiendelea kujikwamua kutoka kwa athari ya mauaji ya halaiki ya 1994  / Photo: AP

Wakati dunia iniadhinisha siku ya kimataifa ya Kumbukizi ya miaka 29 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, Umoja wa Mataifa unaiomba ulimwengu kusimama kidete dhidi ya ongezeko la hali ya kutovumiliana.

"Wacha tuwe macho na tayari kuchukua hatua na tuheshimu kumbukumbu za Wanyarwanda wote walioangamia, kwa kujenga mustakabali wa utu wa haki ya usalama na haki za binadamu kwa wote," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema.

Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda yalianza tarehe 7 Aprili 1994 na yalidumu kwa siku 100. Watu 800,000, wengi wao kutoka kabila la Watutsi waliuawa.

Mwezi Juni 2002 Rwanda ilianza mchakato wake wa uponyaji na upatanisho, kupitia mfumo wa haki mashinani, inayoitwa mfumo wa mahakama ya Gacaca. Kwa muongo mmoja, mahakama za mitaa zilisikiliza kesi ya takribani washukiwa milioni mbili wa mauaji ya halaiki.

Umoja wa Mataifa ulisema "mfumo huo ulichukua jukumu muhimu katika kuendeleza amani, utulivu na maridhiano nchini Rwanda". "Mauaji ya halaiki yasizue tena kichwa chake katika ardhi ya Afrika," alisema Balozi Bankole Adeoye, Kamishna wa Umoja wa Afrika, AU, wa masuala ya kisiasa, amani na usalama.

Je, Rwanda inajimudu vipi miaka 29 baada ya mauaji ya halaiki nchini humo?

  • Rwanda imeanzisha utulivu wa kisiasa na kiusalama tangu 1994 baada ya mauaji ya kimbari
  • Kufikia Desemba 2022, wanawake walikuwa asilimia 61.3 ya bunge la Rwanda na kuifanya kuwa miongoni mwa nchi zenye sehemu kubwa ya wanawake katika bunge duniani.
  • Benki ya Dunia inasema uchumi wa Rwanda uliendelea kupata ukuaji mkubwa mwaka wa 2022 licha ya vikwazo vya kimataifa
  • Imejiunga na nchi chache zinazozalisha chanjo barani Afrika, wakati kampuni ya Ujerumani ya Biontech inapoanzisha kiwanda cha uzalishaji nchini.
  • Rwanda imeendeleza Utalii kama chanzo kikuu cha mapato yake ya fedha za kigeni huku masokwe yake yakiwa kivutio kuu cha kimataifa.
  • Imeanzisha mfumo wa huduma ya afya kwa wote unaojulikana kama ‘Mutuelle de Santé”
  • Rwanda ni mojawapo ya mataifa ya kwanza barani Afrika ambayo imezindua mfumo wa kitaifa wa huduma kupitia ndege zisizo na rubani, yani drone
  • Rwanda ilianzisha mtindo wa maroboti kuwasaidia Wanyarwanda kupata mashauriano kwa urahisi na wataalamu wa matibabu.
  • Mwaka 2008, Rwanda ilipiga marufuku plastiki, shirika la UN-Habitat ilitangaza mji mkuu wa Rwanda, Kigali kama mojawapo ya miji safi zaidi barani Afrika.
  • Katika michezo Rwanda ina uwekezaji mkubwa kupitia ushirikiano na vilabu vya soka vya kimataifa kama vile Arsenal na PSG. Pia imewekeza katika mashindano ya Baiskeli ya Dunia na Mpira wa Kikapu

TRT Afrika na mashirika ya habari