Tokozile Ngwenya, mwandishi vitabu anaielezea fasihi kama kioo kinachosadifu maisha ya wasomaji katika jamii./ Picha: Tokozile Ngwenya  

Na Tokozile Ngwenya

Vitabu vingi kutoka magharibi vilitawala maisha yangu wakati nakua kwenye miaka ya 90, nchini Zambia. Hali ilikuwa hivyo hivyo kwenye maktaba yetu ya shule.

Sikumbuki kukutana na vitabu vya fasihi kutoka kwa waandishi wa Afrika, isipokuwa kile cha "Things Fall Apart" kilichoandikwa na Chinua Achebe, kama kilivyopendekezwa kwetu na walimu wetu wa somo la Kiingereza wakati tuko Sekondari.

Kitabu hicho kilizua gumzo sana nyakati zile, hasa kutokana na mtazamo wake wa kuburudisha. Kama hukupata bahati ya kukutana nacho, ngoja nikupe uhondo kidogo: Kitabu hiki kinazungumzia maisha ya Okonkwo, kiongozi mwenye ushawishi mkubwa aliyekwua hodari katika mchezo wa mieleka.

Yeye na jamii yake wanakutana na ushawishi wa ukoloni wa Ulaya na wamisionari na namna wanavyopokea ushawishi huu. Ni kitabu kizuri ambacho ningependeza kila mtu akisome.

Umoja wa wasoma vitabu

Chama cha Africana Woman Book Club, kilichoanzishwa kwenye robo ya pili ya mwaka 2021, kushughulikia mahitaji ya kijamii. Hili si kundi la wanawake tu, linajumuisha wanachama wa kiume pia.

Kikiwa na wanachama 282, wengi wakiwa ni wasomaji wa vitabu wa Afrika, Ulaya na Asia, chama hicho kinajivunia idadi tofauti ya watu kuanzia tabaka la kati hadi la juu, hasa wenye umri wa miaka 30 hadi 50.

Uchaguzi wa vitabu huzingatia demokrasia kupitia uteuzi na kura za wanachama. Mwaka 2022, klabu hiyo ilipitia vitabu 7 kati ya 8 vilivyoandikwa na Waafrika, na mwaka wa 2023, idadi hiyo ilipanda hadi 8 kati ya 12.

Kikundi cha Africana Woman Book Club kina wanachama kutoka pande tofauti duniani, zikiwemo  Afrika,  Ulaya na Asia./Picha: 

Kulingana na mwanzilishi wa chama hicho Chulu Chansa, mabadiliko haya yanaakisi kuongezeka kwa hali ya kujiamini ndani ya jamii yake, hususani kuingalia fasihi kwa mtazamo wa kiafrika.

Chansa anasisitiza kuwa uhusiano wa simulizi za Kiafrika, huwapa wanachama wake nafasi ya kufahamiana, haswa kwa wale walio ughaibuni.

Anaongeza," vitabu hivi vina uhusiano mkubwa na muktadha wa uandishi wake, unatambua maeneo na hali unazozifahamu, hasa washiriki wetu wengine walioko ughaibuni, wanapata hisia za kuwa nyumbani kwenye kitabu.”

Mahusiano

Kwa mfano, orodha ya vitabu ya kikundi hicho ya mwaka 2023, ilihusisha "Americanah," kilichoandikwa na Chimamanda Ngozi Adichie, ambacho kinaangazia safari ya Ifemelu's kutoka Nigeria kwenda America.

Efemelu, mhusika mkuu katika riwaya hii, alikabiliwa na ubaguzi wa rangi wa aina nyingi kwa mara ya kwanza, alipata uelewa wa changamoto ya kuwa "Mwafrika mweusi".

Aliichukulia Marekani kama tumaini na chanzo utajiri, lakini alikuja kugundua kuwa hiyo yote ilikuwa ni uwongo tu na kwamba hakuna kitu kama; inampasa yeye kubadili matamshi yake, kuelewa siasa za kimarekani ili aweze kuwa sehemu ya nchi hiyo.

Wanachama wa kikundi hicho walijiona wenyewe kwenye mapambano ya Ifemelu, wakipata mwangwi wa uzoefu wao wenyewe ndani ya simulizi. Uwakilishi ni muhimu, na waandishi wa Kiafrika hutoa jukwaa kwa wasomaji kujiona wakionyeshwa katika hadithi wanazotumia.

"Wanachama wanahusiana na wahusika, kutafuta uwakilishi unaowahimiza kuzama katika vitabu vilivyotungwa na Waafrika," Chansa anaeleza.

Nilipata bahati ya kuzungumza na mpenzi wa kazi za fasihi Susan Mukosha Ngombe, ambaye hamu yake iliegemea sana upande wa wanaandishi wa Nigeria. Susan, akivutiwa na akili na maarifa ya waandishi wa Kinigeria, anawashukuru kwa kuimarisha uelewa wake wa nchi na matatizo yake.

Safari yake katika fasihi ya Afrika ilianza na "The Secret Lives of Baba Segi's Wives" kama kilivyoandikwa na Lola Shoneyin, kazi inayoangazia mashinikizo ya kitamaduni na mienendo ya nguvu ndani ya familia katika jamii ya Nigeria.

Ubinadamu wa pamoja

Kazi zingine azipendazo ni pamoja na “I Do Not Come To You By Chance” na Adaobi Tricia Nwaubani, anasema “kitabu hichi kinafurahisha na kinakupa mtazamo wa ulimwengu wa ulaghai.”

Kitabu hiko kimejikita kwa muhusika Kingsley Ibe, mhitimu wa chuo kikuu anayepitia mihangaiko ya kutafuta ajira nchini Nigeria, hali inayomlazimu kuanza kutapeli watu akitumia barua pepe ya mjomba wake, “Cash Daddy”.

Kupitia mitazamo kama ya Susan, ni wazi kwamba vitabu hivi ni kama vioo, vinavyoakisi maisha na mang'amuzi ya wasomaji kila siku.

Kuona tamaduni na mazingira ya mtu yanayoonyeshwa kwenye kurasa kunakuza hisia ya uthibitisho na muunganisho, na hivyo kuimarisha utajiri wa urithi na uzoefu wa pamoja.

Vitabu hukuza mahusiano./Picha: Tokozile Ngwenya

Kuongezeka kwa fasihi iliyotungwa na Kiafrika kunaashiria zaidi ya mwelekeo wa kifasihi tu - inawakilisha jitihada ya pamoja ya utambulisho, kutambuliwa na kusherehekea sauti mbalimbali barani kote na kwingineko.

Kama wasomaji, tunapata utulivu, hamasa na uhakika wa ubinadamu wetu kupitia kurasa za fasihi kutoka Afrika.

TRT Afrika