Kamati inayoshughulikia Kilimo, Maliasili na Utalii kutoka Bunge la Afrika Mashariki (EALA) imeanza mchakato wa kuangazia utekelezaji wa teknolojia ya uhandisi jeni(GMOs) katika baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Mchakato huo wa wiki moja, utapitia baadhi ya sera na sheria katika nchi za Tanzania, Kenya, Burundi na Rwanda.
Nchi zingine ambazo zitatembelewa na kamati hiyo ni pamoja na Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na bunge hilo lenye ofisi zake mjini Arusha, Tanzania, ili iweze kuzifikia nchi zote 6, wabunge hao wamegawanywa katika kamati ndogo ndogo tatu, ambapo kila kamati itatembelea nchi mbili mbili.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Francoise Uwumukiza kutoka Rwanda, ndiye atayeongoza jopo la wabunge hao wakati wa ujumbe huo.
Mchakato huu, ni sehemu ya utekelezaji wa itifaki ya Afrika Mashariki unaohusiana na ushirikiano katika maendeleo ya sekta ya kilimo, wenye kulenga kufikia usalama wa chakula na kuchagiza uzalishaji wa sekta hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC).
Katika ujumbe huo, wabunge wa EALA watakuwa na majadiliano ya kina na wadau wa kilimo kutoka sekta ya umma na binafsi pamoja na kutoa mapendekezo yanayofaa kwa Baraza la Mawaziri wa EAC kuhusu GMOs na hatua sahihi zitakazofaa kuchukuliwa na nchi wanachama.
Sera ya Kilimo na Maendeleo Vijijini ya EAC, maarufu kama EAC ARDP, inalenga kupata uhakika wa chakula kupitia kuongezeka kwa uzalishaji, usindikaji, uhifadhi na upatikanaji wa masoko.