Ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa ilitangaza kuundwa kwa uchunguzi huru utakaoongozwa na jaji mstaafu   / Photo: AP

Marekani inasema Afrika Kusini mwaka jana iliipatia Urusi silaha na risasi kwa vita vya Ukraine -lakini haikutoa ushahidi kuunga mkono madai hayo.

Silaha hizo zilipakiwa kwenye meli ya kivita ya Urusi iliyokuwa imetia nanga katika kambi ya wanamaji mjini Cape Town, balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini Reuben Brigety alisema.

"Miongoni mwa mambo tuliyoyabaini ni pamoja na kupandishwa kwa meli ya mizigo katika kambi ya jeshi la majini ya Simon's Town kati ya tarehe 6 hadi 8 Disemba, 2022, ambayo tuna uhakika ilipakia silaha na risasi kwenye meli hiyo huko Simon's Town ilipokuwa ikirejea Urusi. "Bw Brigety aliambia wanahabari siku ya Alhamisi.

Kufuatia madai hayo, ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa ilitangaza kuundwa kwa uchunguzi huru utakaoongozwa na jaji mstaafu. "Huduma za kijasusi za Marekani zitatoa ushahidi wowote ulio nao," msemaji alisema.

Katika mkutano wake na vyombo vya habari, balozi wa Marekani alisema "ataweka dau maisha yake" juu ya usahihi wa taarifa za kijasusi kwenye madai ya ugavi wa silaha, na akaongeza kuwa itakuwa "kosa kudharau wasiwasi uliopo Washington".

Alisema suala hilo tayari limezungumzwa na wajumbe wa Afrika Kusini waliotembelea Marekani hivi karibuni.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi kadhaa za Kiafrika ambazo zilichukua msimamo usiofungamana na upande wowote katika vita vya Ukraine na kujiepusha na kura ya Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi huo.

Mnamo Februari iliandaa mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Urusi na Uchina ambayo ilikosolewa kama uidhinishaji wa uvamizi wa Ukraine.

Nchi hiyo inatazamiwa kuwa mwenyeji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin mwezi Agosti wakati wa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa ya Brics.

TRT Afrika