Afrika Kusini inakaribisha makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas baada ya miezi 15 ya mauaji ya halaiki yaliyofanywa na Israeli dhidi ya Gaza baada ya Hamas na makundi mengine yenye silaha kushambulia Israel.
Kundi la Palestina la Hamas na Israeli zimefikia makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza na pia kukubaliana ubadilishanaji wa wafungwa, hii ni kulingana na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Qatar.
Msuluhishi huyo wa mgogoro huo, alisema siku ya Jumatano kuwa awamu ya 42 ya kusitisha mapigano hayo itafanyika Januari 19.
"Afrika Kusini inataka kutekelezwa kwa amani na haki ya kudumu ambayo inahakikisha haki za binadamu za Wapalestina na Waisraeli zinalindwa na kukuzwa," taarifa iliyowekwa mitandaoni na Ronald Lamola, ambae ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini.
Afrika Kusini imesema makubaliano ya kusitisha mapigano ni " hatua muhimu ya kwanza kuelekea kumaliza mzozo mkali wa kibinadamu unaowakabili Wapalestina milioni 2.3 katika Ukanda wa Gaza."
Imependekeza kuwa usitishwaji wa mapigano lazima uweke msingi wa amani ya haki ambayo inapaswa kujumuisha uanzishwaji wa taifa la Palestina.
"Mamlaka ya Palestina na uadilifu wa eneo lazima udumishwe. Ni muhimu kwamba hakuna ardhi iliyotwaliwa Gaza au Ukingo wa Magharibi kufuatia kusitishwa kwa mapigano, na kwamba upanuzi wa makazi haramu ukomeshwe," taarifa ya Afrika Kusini ilisema.
Mnamo Disemba 2023, Afrika Kusini ilianzisha kesi dhidi ya Israeli, katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, ikidai ukiukaji wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari kuhusiana na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Nchi kadhaa zimejiunga na kesi hiyo, zikiwemo Nicaragua, Colombia, Libya, Mexico, Palestina, Uhispania na Uturuki, na sasa Cuba pia imejiunga na kesi hiyo.
"Kwa mujibu wa maamuzi yanayofuatana ya ICJ, hatua za muda zilizowekwa na ICJ lazima zifuatwe na mamlaka inayokalia. Sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu lazima ziheshimiwe na kuzingatiwa," imesema Serikali ya Afrika Kusini.