Afrika Kusini imetangaza kufunga kwa muda kivuko cha mpaka wake na Msumbiji, ambacho huwa na shughuli nyingi kutokana na ghasia zinazoendelea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi nchini Msumbiji.
Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka ya Afrika Kusini ilisema ilipokea taarifa za magari kuchomwa moto upande wa Msumbiji wa Bandari ya Lebombo.
"Kutokana na matukio yenye kuhatarisha usalama, tumechukua uamuzi wa kufunga mpaka katika bandari ya Lebombo hadi tutakapo taarifiwa baadaye," alisema Micheal Masiapato, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka (BMA) katika taarifa yake ya Jumanne jioni.
Msumbiji imeshuhudia wimbi la maandamano tangu mwishoni mwa Oktoba baada ya Daniel Chapo kutoka chama cha Frelimo kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 9.
Kiwango cha juu cha usafiri
Chapo, mwenye umri wa miaka 47, alishinda kwa asilimia 71 ya kura dhidi ya mpinzani wake wa karibu Venancio Mondlane kutoka chama cha Podemos, aliyepata asilimia 20.32 ya kura.
Mondlane amekuwa akihamasisha maandamano kama ishara ya kupinga matokeo hayo ambayo ameyaita kuwa ni ya "udanganyifu."
Eneo la mpaka wa Lebombo lifahamika kwa pilikapilika nyingi, ambazo huusisha wafanyabiashara na wasafiri kuvuka pande mbili za nchi hizo.
Kulingana na BMA, uamuzi wa kufunga kwa muda mpaka huo ni kama tahadhari ya kuhakikisha usalama wa wasafirishaji, wasafiri, wafanyabiashara katika bandari hiyo.
"Tunashauri wadau wote kusitisha safari kupitia Bandari ya Lebombo hadi watakapotangazwa tena, njia mbadala za kwenda Msumbiji zitumike tu pale inapolazimika, ila kwa sasa, tusubiri hadi hali itakapotengemaa," aliongeza Masiapato.
Katika hatua nyingine, mamlaka za Afrika Kusini zinasema kuwa zimeendelea kutoa msaada kwa maafisa saba kutoka upande wa Msumbiji ambao wameomba hifadhi upande wa Afrika Kusini.