Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikisikiliza kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israeli./ Photo: AFP

Mwaka mmoja tangu kuanza kwa mashambulizi dhidi ya watu wa Palestina, Afrika Kusini imeungana na jamii ya kimataifa kushutumu kuendelea kwa mashambulizi hayo.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini itawasilisha kumbukumbu muhimu katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ambazo ni ushahidi wa kina kuthibitisha kuwa Israeli inatekeleza mauaji ya kimbari huko Palestina.

Nchi hiyo Iliishitaki Israeli katika Mahakama ya Kimataifa Januari 2024.

" Baadaye mwezi huu, tutawasilisha kumbukumbu, ambayo ni kesi kamili ya msingi ya Afrika Kusini kulingana na ushahidi, katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Kumbukumbu hizo ni ushahidi wa kina kuthibitisha kuwa Israeli inatenda uhalfu wa mauaji ya halaiki huko Palestina," Rais Ramaphosa amesema katika taarifa.

Rais Ramaphosa ameongezea kuwa ni muhimu kwa Israeli kutii maagizo ya Mahakama ya Januari 26, Machi 28 na Mei 24 mwaka huu.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini itawasilisha ushahidi wa kina kuthibitisha kuwa Israeli inatekeleza mauaji ya kimbari huko Palestina/Picha : Reuters 

" Wengi waliouawa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni raia wa Palestina, wengi wao wakiwa wanawake na watoto katika Ukanda wa Gaza ambao umezingirwa. Inatisha kuwa Wapalestina zaidi pia wanauawa katika Ukingo wa Magharibi kutokana na shughuli za kijeshi za Jeshi la Ulinzi la Israeli," taarifa yake imeongeza.

Kulingana na kiongozi huyo wa Afrika ya Kusini, hali inazidi kuwa mbaya kutokana pia na mashambulizi ya Israeli dhidi ya Lebanon na Iran, licha ya uwepo wa juhudi za jumuiya ya kimataifa za kumaliza mgogoro huo.

" Israeli imeapa kulipiza kisasi dhidi ya Iran huku Iran ikiazimia kujibu mapigo. Wasiwasi mkubwa unatanda kadiri hali inavyozidi kuwa mbaya katika eneo la Mashariki ya Kati kwani inatishia kulitumbukiza eneo hilo katika vita ambavyo vitakuwa mzigo mkubwa kwa raia."

Mbali na kutaka mashambulizi dhidi ya Gaza kumalizika, Rais Ramaphosa amesema kuna hitaji la dharura la kuchukua ili kuepusha njaa na magonjwa miongoni mwa wakazi. Kwa mujibu wa Ramaphosa rasilimali nyingi zinahitaji kuelekezwa Gaza ili kuanza kujenga upya miundombinu, makazi, huduma za kijamii, uzalishaji wa kilimo na shughuli za kiuchumi.

TRT Afrika