Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Kura zimehesabiwa nchini Afrika Kusini na chama tawala cha Africa National Congress ANC kimeshindwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Hii inamaanisha kuwa, chama hicho tawala kikongwe nchini humo kitashindwa kuunda serikali hivyo kulazimika kutengeza serikali ya mseto au muungano na vyama vyengine.
ANC inayoongozwa na Cyril Ramaphosa imepata 40% ya kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita.
Hii ina inamaanisha nini?
Chama chochote kilichoshiriki katika uchaguzi uliopita nchini Afrika Kusini, ili kiweze kuunda serikali, kilitakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Tofauti na mataifa mengine, ambapo rais hupigiwa kura moja kwa moja katika uchaguzi mkuu, Afrika Kusini, wabunge wa chama ndio humchagua rais baada ya wao kuchaguliwa na wananchi.
Wananchi wanachagua wajumbe wa Bunge la Kitaifa, ambao kisha wanamchagua rais kwa kura nyingi.
Bunge la nchi hiyo, lina jumla ya viti 400, na chama kinachoibuka na zaidi ya wabunge 201 ndicho kinachomchagua rais na hatimae kuunda serikali.
Zaidi ya vyama 50 vilishiriki katika uchaguzi huo mkuu, na angalau vinane vilipata sehemu kubwa ya kura.
Lakini kuna vyama vitatu vyenye uwezo wa kuunda serikali na ANC kutokana na matokeo ya Tume ya Uchaguzi.
Chaguo la wazi ni chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, DA, iliyotapa asilimia 21.81 ya kura zilizopigwa. Kinaongozwa na John Steenhuisen, kiongozi pekee wa kizungu kati ya vyama vinne vikuu.
Iwapo ANC ikiungana nayo watakuwa na viti vya kutosha Bungeni kutawala kwa urahisi.
Lakini DA imekuwa ikikosoa vikali sera za ANC kwa miaka mingi hivyo muungano huu unaweza usiwe rahisi, licha ya wote kusema wako tayari kwa majadiliano.
Chaguo jengine ni ANC kuungana na chama kinachoongozwa na rais wa zamani Jacob Zuma kinachoitwa chama cha uMkhonto WeSizwe au MK, kilichopata asimilia 14.58 ya kura.
ANC pia inawezakuungana na chama cha MK na chama cha Economic Freedom Fighters, EFF kinachoongozwa na Julius Malema ambacho kilipata asilimia 9.52 ya kura.
Wataalamu hata hivyo, wanasema hii inaweza kuharibu taswira ya Afrika Kusini na wawekezaji wa kigeni kwani vyama vya MK na EFF wote wameahidi kufanya migodi muhimu ya dhahabu na platinamu ya Afrika Kusini na benki kuu kuwa chini ya taifa.
Kura za 2024 Afrika Kusini zimeashiria mengi kisiasa. Kati ya watu milioni 27.7 waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 16.2 pekee ndio walipiga kura siku ya uchaguzi.
Hii inalinganishwa na asilimia 58.64 ni idadi ndogo zaidi kuwahi kutokea katika historia ya miaka 30 ya kidemokrasia ya Afrika Kusini.
Chama cha ANC kilichoikomboa Afrika Kusini kutoka mfumo wa ubaguzi wa rangi wa utawala wa wazungu wachache mwaka 1994, chini ya rais wake wa kwanza Muafrika Nelson Mandela.
Wakati ANC ikijianda kutafuta mshirika katika serikali ya muungano, kila chama kinatoa masharti yake ya muungano.ANC itaunda serikali na chama kipi, ndio swali lililopo sasa hivi.