Afrika Kusini ilitangaza matokeo yake ya mwisho ya uchaguzi Jumapili, huku Chama cha African National Congress (ANC) kikipata viti 159 tu katika Bunge la Kitaifa kati ya 400.
Hii inathibitisha kwamba hakuna chama kilichoshinda na kura nyingi kuweza kuunda serikali peke yake, huku mazungumzo ya muungano yameanza ya kuunda serikali ya mseto.
''Kile ambacho uchaguzi huu umefanya ni kwamba watu nchini Afrika Kusini wanatarajia viongozi wao kufanya kazi pamoja ili kukidhi mahitaji yao,'' alisema Ramaphosa katika hafla ya kutangazwa mshindi.
Chama cha African National Congress tayari kilikuwa kimepoteza kura zake nyingi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30, baada ya zaidi ya 99% ya kura kuhesabiwa kufikia Jumamosi na kuonyesha hakingeweza kuvuka asilimia 50.
Wamepata kura chini ya zilizotarajiwa
ANC ilipata karibu asilimia 40 ya kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita kulingana na matokeo ya mwisho, ambayo ni sehemu kubwa zaidi.
Ramaphosa alikiri kuwa matokeo hayo yamebeba ujumbe mzito kutoka kwa wananchi wa Afrika Kusini, yakitathmini utendakazi ya serikali yake.
''Uchaguzi huu umethibitisha tena kwamba kujenga Afrika Kusini kwa ajili ya wote inasalia kuwa dhamira kuu ya nchi yetu. Kama viongozi wa vyama vya siasa, tumesikia sauti za watu wetu, na lazima tuheshimu matakwa yao,'' Ramaphosa aliongeza.
Bila wingi wa kura, itahitaji kufanya muungano na chama au vyama vingine kwa mara ya kwanza ili kutawala Afrika Kusini na kumchagua tena Rais Cyril Ramaphosa kwa muhula wa pili.
Nini kinafuata?
Uchaguzi wa kitaifa wa Afrika Kusini huamua ni viti vingapi kila chama kimepata bungeni, na wabunge humchagua rais baadaye.
ANC ilisema mapema Jumapili kwamba ilikuwa inaanza mazungumzo yake na vyama vyote vikuu katika jaribio la kuunda serikali ya kwanza ya mseto ya kitaifa ya Afrika Kusini.
Katibu Mkuu wa ANC Fikile Mbalula alisema, chama hicho kiko tayari kwa mazungumzo yote, hata na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, ambacho kimeongoza kwa ukosoaji wa ANC kwa miaka mingi, huku wachambuzi wengi wakisema muungano huo utakuwa thabiti zaidi kwa Afrika Kusini.