Chama tawala cha Afrika Kusini, Africa National Congress, ANC, kimefanya makubaliano na vyama viwili hadi sasa kuunda serikali ya muungano.
Katika uchaguzi mkuu wa Mei 29, 2024, chama cha ANC kilipata asilimia 40 ya kura hivyo kushindwa kuunda serikali. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, ili chama kiweze kuunda serikali, kinatakiwa kupata angalau asilimia 51 ya kura.
Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance kilichopata asilimia 21 kwa kura za Mei, ametangaza rasmi kuwa chama cha DA kitakuwa katika serikali mpya.
"Kufuatia kutiwa saini kwa makubaliano na viongozi wa vyama husika - ikiwa ni pamoja na DA, Inkantha Freedom Party, IFP na ANC - DA sasa itaingia katika serikali ya kitaifa, pamoja na serikali ya mkoa katika majimbo ya Gauteng na KwaZulu-Natal," kiongozi wa chama cha DA John Steenhuisen amesema katika hotuba yake.
Chama cha ANC kinasema kimefanya majadiliano na vyama vyote 17 ambavyo vilihusika.
"Tunashirikisha vyama vyote vya siasa kwa heshima, hadi kufikia hatua ambapo ANC inajihusisha na chama chenye kiti kimoja ...Wananchi wamezungumza na wanataka tushirikiane," Fikile Mbalula, Katibu Mkuu wa chama cha ANC amesema.
Wananchi wengine wamesema ANC kuungana na DA ambacho ni chama cha wazungu ni kama kuirejesha Afrika Kusini katika uongozi wa ubaguzi wa rangi.
Lakini kulingana na matamshi ya kiongozi wa chama cha EFF, Julius Malema, chama chake ambacho kilipata asilimia 9 katika uchaguzi mkuu, hakijakubali kuunda serikali na ANC.
"Watu wa Afrika Kusini lazima wameze walichoamua kutafuna... Waliamua kutafuna 40% ya ANC... Walichagua ukosefu wa umeme na Ramaphosa, kiwango cha juu kabisa cha ukosefu wa ajira na ubaguzi wa rangi," Malema amesema katika mkutano wa waandishi wa habari.
"Kuanzia sasa na kuendelea unaposema kuna mbaguzi wa rangi katika kazi yetu, tunaangalia historia yako ya mtandao wa X kama umekuwa ukituma ujumbe kwenye ANC au DA, nenda kapigane na hao wazungu pekee yao," Malema amesema.
Wabunge wanatazamiwa kumchagua rais leo huku bunge likikutana. Vyama vya ANC na DA kwa pamoja wana wabunge wengi ambao watamwezesha rais wa sasa Cyril Ramaphosa wa mwenye umri wa miaka 71 kurejea kwa muhula wa pili.