Afcon 2023: safari yashika kasi huku mataifa yakitafuta tiketi  kwenda  Côte d'Ivoire.

Afcon 2023: safari yashika kasi huku mataifa yakitafuta tiketi  kwenda  Côte d'Ivoire.

Mataifa ya Afrika yanapambana katika mechi za kufuzu fainali ya kuvishwa taji la ubingwa wa Afrika kwenye fainali ya Januari mkwani.
Bingwa wa sasa wa Afcon 2022 ni Senegal waliowalaza watani wao Misri 

Raundi ya tano ya mechi za mchujo itachezwa wikendi ya 20 Juni huku mataifa kadhaa yakitaka kujihakikishia nafasi kwenye fainali ya michuano ya mataifa bora barani Afrika Januari ijayo.

Nigeria, watakuwa wanatafuta kurejesha matumaini baada ya kupoteza uongozi wa Kundi lao dhidi ya Guinea Bissau, watakapokuwa ugenini kumenyana na Sierra Leone siku ya jumapili.

Super Eagles wanahitaji alama moja pekee kufuzu. Wenyeji Sierra Leone, wanaoshikilia nafasi ya tatu, watalazimika kuilaza Nigeria ili kufufua matumaini yao ya kusonga mbele. Sao Tome & Principe hawana budi kufunganya virago baada ya kufanikiwa alama moja tu kufikia sasa.

Katika Kundi B, ushindani mkali unatarajiwa kati ya Cape Verde, eSwatini na Togo baada ya Burkina faso kufuzu huku wakiwa na mechi mbili bado kapuni.

Aidha viongozi wa kundi C, Namibia, wanahitaji alama moja dhidi ya watani wao kutoka Afrika Mashariki Burundi, kwenye jedwali hilo lenye timu tatu pekee.

Fainali za kombe la taifa bingwa Afrika zitachezwa mwezi Januari 2024 nchini Cote d'Ivore Picha : Nigeria Football Federation

Katika kundi D, Mabingwa mara saba, Misri, walijihakikishia nafasi kwa kuilaza Guinea 2-1 na kuzoa alama 3 muhimu huku ikifikisha jumla ya alama 12. Hata hivyo, Malawi na Ethiopia wana kibarua kigumu kwani wana alama tatu pekee licha ya kucheza mechi tatu kila mmoja.

Mabingwa watetezi Senegal, walioweka historia kwa kuinua taji hilo kwa mara ya kwanza 2022, nchini Cameroon tayari wametinga fainali za Afcon 2023 kulitetea taji lao kwa kuwa na rekodi ya 100% ya ushindi mara nne katika mechi zake nne.

Senegal inafuatwa katika kundi hilo na Msumbiji walio katika nafasi ya pili kwa pointi nne, Rwanda ya tatu na alama tatu na Benin wanaoshikilia mkia wakiwa na alama mbili.

Kundi E, lenye mataifa ya Ghana, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Angola, limegeuka kuwa kundi la maajabu huku timu zote zikiwa na nafasi ya kufuzu baada ya matumaini ya Madagascar kudidimia. Ghana ndio wanaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nane, ikifuatwa na CAR ya pili ikiwa na pointi saba nayo Angola ikiwa katika nafasi ya tatu na pointi tano.

Angola watakuwa ugenini dhidi ya CAR huku Madagascar wakiikaribisha Ghana mjini Antananarivo. Ghana na CAR zote zitahitaji ushindi katika raundi hii ili zifuzu kwa Afcon 2023 huku Angola wakiwa na lazima kushinda.

Katika Kundi F, Algeria tayari wamefuzu, huku ushindani mkali ukisubiriwa kati ya majirani wa Afrika Mashariki Tanzania na Uganda. Tanzania watachuana na Niger nayo Uganda wakikwatuana na Cameroon.

Timu za Afrika Mashariki, Tanzania na Uganda watapambana katika Kundi F Picha : TFF Twitter

Wakati huo huo, Sudan Kusini watakuwa wenyeji wa Gambia huku wakihitaji ushindi kwenye pambano lao la nyumbani kufufua matumaini yao, katika raundi ya mwisho ya mechi za kufuzu.

Viongozi wa kundi G, Mali watahitaji sare tu watakapocheza ugenini Brazzaville dhidi ya Congo inayoshikilia nafasi ya pili.

Katika kundi H, wenyeji wa mashindano ya Afcon 2023, Côte d'Ivoire, tayari wamefuzu kwa mchuano huo na kuacha kibarua kwa Zambia na Comoros kuwania tiketi moja pekee iliyosalia kwenye kundi hilo.

TRT Afrika